Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutotoka
nje ya nchi katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ili
ashughukie maandalizi yake ipasavyo.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho,
Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya
Nzega katika ziara yake ya siku 10 mkoani Tabora.
“Hadi sasa hakuna matumaini kwamba Uchaguzi Mkuu
utafanyika kama ilivyopangwa, hivyo Rais lazima awepo nchini aangalie
wapi tumekwama na aingilie kati kunusuru mchakato huo,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kuwa makini, vinginevyo uchaguzi utavurugwa.
“Tunatoa ushauri kwa Rais Kikwete kusitisha safari
zake za nje ya nchi ili aweze kuhakikisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu
yanakamilika kwa wakati, vinginevyo mambo yatavurugika,” alisema Profesa
Lipumba.
Mwenyekiti huyo wa CUF, pia alitoa wito kwa watu
wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura na
asiwepo mtu wa kuachwa kuandikishwa kwa kisingizio chochote.
Hata hivyo, aliilaumu Serikali kwa kile
alichokieleza kuwa imeipangia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), fedha
kidogo kwa ajili ya uchaguzi, jambo ambalo linaashiria kuwa hakuna
maandalizi ya maana ya Uchaguzi Mkuu.
Safari za Rais nje
Profesa Lipumba alisema safari za Rais Kikwete
nje ya nchi zinagharimu kati ya Sh5 bilioni na Sh10 bilioni. Alisema
hayo ni matumizi mabaya hasa kwa Serikali ambayo pia haiwajibiki
kukusanya kodi ipasavyo.
Profesa Lipumba pia aliishangaa Serikali kwa kutoa
misamaha ya kodi kwa kampuni mbalimbali, bila kuwa na vyanzo mbadala
vya mapato kwa ajli ya kuendeshea shughuli zake, akisema hatua hiyo ni
hatari kwa ustawi wa nchi.
Profesa Lipumba alisema kuwa kiinua mgongo cha
Sh230 milioni kwa kila mbunge ni sehemu ya matumizi ya fedha za Serikali
na ndiyo kinachosababisha mivutano mikali wakati wa kura za maoni ndani
ya CCM.
“Mkitaka maisha mazuri iondoeni Serikali ya CCM
isiyowajali wananchi wake na yenye matumizi mabaya ya fedha zenu
wananchi,” alisema.
Post a Comment