Lowassa: Asiyenipenda CCM ahame

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.
Kuhama CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Kimya miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.
“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza, askofu mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu. Nilichagua kuwa kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza, ningezungumza ningeweza kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo ambayo hayapo.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake.... sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.

Post a Comment

Previous Post Next Post