Tabora. Siku kadhaa tangu Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kuwatahadharisha wajumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC), ya chama hicho kwamba wanapaswa kumteua mgombea
wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama hicho, Chama cha Wananchi
(CUF), kimesema kauli hiyo haina ukweli.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
(pichani) amesema hakuna mtu anayefaa kuwa Rais ndani ya CCM, kwa kuwa
mfumo wa chama hicho hauruhusu uadilifu.
Profesa Lipumba alisema hayo jana alipokuwa akihutubia wakazi wa Kijiji cha Kayombo wilayani Nzega.
Alisema ndani ya CCM, kuna tatizo la kimfumo
ambalo hata akitokea mtu mwadilifu akawa rais, bado atavurugwa na mfumo
uliopo na kuwa fisadi.
“CCM kimekosa mfumo wa uadilifu hivyo hakiwezi
kutuletea kiongozi wa nchi, kwani hata akitokea mtu mwadilifu akashinda,
bado atavurugwa na mfumo huo wa kifisadi,” alisema Profesa Lipumba.
Sifa za Rais
Profesa Lipumba ambaye yuko mkoani Tabora kwa
ziara ya kuhamasisha wananchi wajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura, alisema kwa hali ilivyo, Tanzania inahitaji Rais mwadilifu
ambaye kimsingi, hawezi kutokea CCM.
Alisema uongozi wa CCM hauthamini dira ya Taifa na
tatizo hilo ndilo linalofanya wananchi wawe na maisha magumu kwa kukosa
uhakika wa matibabu, elimu bora na chakula.
Profesa Lipumba alisema wananchi hawapati matibabu
ya uhakika kwa kuwa zahanati na hospitali hazina dawa. Lakini hayo
yakiendelea, viongozi wanakwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Elimu nayo inatolewa kwa ubaguzi. Watoto wa
maskini wanasoma sekondari za kata ambazo hazina walimu wala vitabu na
watoto wa matajiri wanasoma shule zenye walimu na vitabu,” alisema.
Profesa Lipumba alibainisha kwamba endapo CUF
itaingia madarakani, wananchi watapata haki mbalimbali zikiwamo za
elimu, afya na haki nyingine tofauti na ilivyo sasa.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa uchaguzi ndiyo
fursa ya kuitoa CCM madarakani na kwamba hawawezi kupiga kura kama
hawajajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura
إرسال تعليق