Mvua za
masika zinazoendelea kunyesha Visiwani Zanzibar zimesababisha hasara kubwa ikiwemo
upotevu mali na mifugo, uharibifu wa miundombinu pamoja na kusababisha vifo vya
watu.
Hayo
yamweelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe.
Mohamed Aboud Mohamed wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na athari za
mvua hizo katika ukumbi wa Karume House,
Mjini Zanzibar.
Amesema
mvua hizo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mjini
Magharibi na kupelekea athari kubwa katika maeneo hayo ikiwemo vifo vya watu,
uharibifu wa nyumba za makaazi na upotevu wa mali na mifugo, ambapo hadi sasa
watu wawili (2) ambao ni Nd. Juma Hamad (25) mkaazi wa Mwanakwerekwe na mtoto
mmoja (1) mkaazi wa Kinuni anaekisiwa kuwa na miaka 8 wamepoteza maisha wakiwa wote
wawili ni kutoka Wilaya ya Magharibi Unguja.
Aidha Waziri
Aboud amesema kuwa maiti ya mtoto imeshapatikana na kuzikwa jana Tarehe 3/5/2015
na maiti ya Nd. Juma Hamad bado haijapatikana na juhudi za kumtafuta
zinaendelea.
Amefahamisha
kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo ni pamoja na Magomeni, Jang’ombe,
Nyerere, Sebleni, Sogea, Mwanakwerekwe, Welezo, Kisauni, Tomondo, Mombasa, Kinuni,
Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae, Bububu na Kwaalinato, ambapo maeneo yote hayo
yanapatikana ndani ya Mkoa wa Mijini Magharibi.
Ametanabahisha
kuwa, kwa vile mvua bado zinaendelea kunyesha ni vyema wananchi wakachukua
tahadhari ili kujiepusha na athari zaidi zinazoweza kujitokeza, ikiwemo wazazi
kuangalia watoto wao na kuhakikisha hawachezi karibu na maeneo yanayotuama
maji, kwa wale wanaoishi mabondeni ni vyema wakahama sehemu hizo.
Waziri Aboud
pia amewataka wananchi waliochimba mashimo katika maeneo ya makaazi wawe
waangalifu kwa kuyafunika haraka iwezekanavyo , kuchemsha maji wanayoyatumia,
kuhifadhi chakula ili kuepukana na maradhi ya miripuko pamoja na kufuata kanuni
za afya ikiwemo usafi binafsi na maeneo yanayowazunguka.
Vilevile
amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwani Serikali itaendelea
kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa hali ya maisha kwa wananchi hao inarudi
kama kawaida pamoja na kuwapa pole wale wote waliopoteza jamaa na mali zao.
Na Abdulla Ali-Maelezo Zanzibar .
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO
ZANZIBAR
إرسال تعليق