Fahmi Nasoro Dovutwa ni Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha
United Peoples Democratic Party (UPDP). Alizaliwa Februari 27, 1957
mjini Kisarawe mkoani Pwani (Amefikisha miaka 58 Februari mwaka huu).
Dovutwa alianza elimu yake ya msingi mwaka 1967
katika shule ya msingi Zanaki hadi alipohitimu mwaka 1974 alipoendelea
na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Azania ambako alihitimu
mwaka 1977.
Rekodi za elimu za Dovutwa zimekuwa “kizungumkuti”
kupatikana. Hata taarifa zake binafsi alizotoa kwa ajili ya rekodi za
Bunge Maalum la Katiba zinasisitiza kuwa ameishia kidato cha nne.
Juhudi za kumpata yeye mwenyewe ili akamilishe
rekodi zake hazikufua dafu na ni yeye peke yake tangu nianze kufanya
uchambuzi wa watu wanaotajwa kuwania urais, ambaye hakutoa ushirikiano
kabisa ili kunifanya nipate rekodi zake sahihi. Hata hivyo hilo haliwezi
kunizuia kumchambua.
Watu wa karibu yake wamenijulisha kuwa kwa muda
mrefu amekuwa akijishughulisha na kazi za ujasiriamali katika soko la
Magereza jijini Dar es Salaam hadi baadaye alipochaguliwa kuongoza chama
cha UPDP ambacho yeye ni mwenyekiti hadi sasa.
Mwaka 2014, alikuwa ni miongoni mwa Watanzania
waliopata fursa ya kuteuliwa na Rais wa Tanzania kupitia kundi la vyama
vya siasa, na kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba lililofanya kazi
yake mjini Dodoma na kukamilisha Katiba Inayopendekezwa ambayo hata
hivyo imeligawa taifa katika vipande viwili. Dovutwa ameoa na ana
watoto.
Mbio za ubunge
Katika historia ya kisiasa ya Dovutwa, hakutoa pia
rekodi zinazoonyesha kama aliwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote
na hata nilipozitafuta sikufanikiwa kuzipata.
Mbio za urais
Kiongozi huyu alijitosa katika mbio za urais mwaka
2010 akitumia tiketi ya chama chake cha UPDP. Katika uchaguzi ule ambao
Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza kwa ushindi wa asilimia 62.83,
akifuatiwa na Willibroad Slaa aliyekuwa na ushindi wa asilimia 27.5, na
Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akiwa na asilimia 8.28, Dovutwa aliibuka
katika nafasi ya mwisho akiwa na asilimia 0.16 ya kura zote kwa kupitwa
na Peter Mziray wa APPT (asilimia 1.15), Hashim Rungwe wa NCCR (asilimia
0.31), na Mutamwega Bhatt wa TLP aliyekuwa na asilimia 0.21 ya kura
zote.
Katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dovutwa
hajatangaza popote kuwa atagombea tena nafasi ya urais lakini duru za
kisiasa ndani ya chama hicho ikiwamo kutoka kwa baadhi ya viongozi
waandamizi, zimenieleza kuwa anapewa nafasi kubwa ya kugombea tena.
Post a Comment