Sitti Mtemvu, Miss Tanzania wa kwanza katika
historia ya shindano hilo kutema taji la urembo, anazindua kwa mpigo
'shirika' lisilo la kiserikali la misaada ya kijamii, kitabu na kipindi
cha TV jijini Dar es Salaam leo.
Lazima tukubali, Nipashe, kwamba kitendo cha Sitti ambaye
alilazimika kutema taji hilo mwaka jana baada ya kupata kashfa ya
kupunguza umri wake ili aweze kushiriki shindano la Miss Tanzania, cha
kuanzisha taasisi ya misaada kwa jamii, ni cha kuungwa mkono kwa
asilimia 100 kutokana na uwepo wa watu wengi wenye mahitaji nchini.
Lakini, tunasikitika Nipashe, pamoja na nia njema ya mrembo huyo
katika kuelekeza nguvu, uwezo na nafasi yake kwenye jamii katika kutoa
chozi kwa ajili ya watu wenye mahitaji, hafla hii inakuja wakati ambao
jina la mfadhili huyo linazidi kuchukiwa ndani ya jamii kadri siku
zinavyokwenda mbele.
Ikumbukwe kuwa tuhuma za Sitti za kughushi umri ili ashiriki katika
shindano la Miss Tanzania la mwaka jana zimeacha majanga ambayo mengi
hayawezi kurekebishika tena.
Tuhuma zimeacha majanga nyuma ambayo mengi hayawezi kurekebishika
tena kwa sababu, kwanza, shindano lenyewe la Miss Tanzania
limesimamishwa kwa miaka miwili pamoja na makosa mengine, kuwapo kwa
rekodi za vyeti viwili vya kuzaliwa vya Sitti vyenye kumuonyesha
alizaliwa miaka miwili tofauti.
Kusimamishwa kwa Miss Tanzania kunaweza kuonekana kama baa
lililowakumba Hashim Lundenga na Prashant Patel tu kutokana na fainali
za shindano hilo kuwa moja ya matukio makubwa ya burudani nchini la kila
mwaka lenye udhamini mnono.
Lakini ikumbukwe shindano la Miss Tanzania si tu ni chanzo cha
ajira, hata kama ya muda, kwa washiriki, waandaaji na wasanii bali pia
ni fursa ya biashara kwa wamiliki wa kumbi mbalimbali kuanzia ngazi za
vitongoji mpaka taifa.
Aidha, ni wazi, kama Mamlaka ya Kodi (TRA) ni makini vya kutosha,
kuna kiasi cha pato la taifa ambacho kitakuwa kimekosekana katika misimu
mwili hii na yote, inasikitisha, ni kutokana na tuhuma za Sitti za
udanganyifu wa umri.
Kibaya zaidi, madhara ya tuhuma za udanganyifu wa umri za Sitti
hayaishii katika ngazi hizo za jamii na taifa kwa ujumla tu bali hata
familia.
Tunasema madhara ya tuhuma za udanganyifu wa umri za Sitti yanagusa
pia ngazi ya familia baada ya Ofisi ya Msajili wa Vifo na Vizazi (Rita)
hivi karibuni kufafanua kuwa wafanyazi kadhaa wa wakala huyo ama
walifukuzwa kazi, kusimamishwa au kupewa barua za karipio kali kutokana
na tukio hilo.
Watoto na wategemezi wa mfanyakazi yeyote wa Rita aliyefukuzwa kazi
kutokana na tuhuma za kusaidia kupatikana kwa cheti cha kughushi cha
Sitti, basi, haitashangaza kama watakuwa wateja wa shirika na chozi vya
mrembo huyo.
Tumpongeze tena Sitti kwa kuanzisha kitengo ambacho kinaweza kuja
kuwa kimbilio la waathirika wa matendo yake ya awali endapo itathibitika
mahakamani.
Lakini baada ya Rita kutimiza wajibu wake bila hofu wala upendeleo,
tuchukue fursa hii, Nipashe, kutaka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam nalo litimize wajibu wake katika kuhakikisha mrembo huyo
anafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zilizopo.
Kuacha Miss Tanzania, warembo, mawakala, wasanii, wamiliki kumbi za
starehe, TRA na wafanyakazi na familia za wafanyakazi wa Rita wakiwa
wahanga wa kitendo ya Sitti huku binti mwenyewe akipeta ndani ya jamii,
ni dalili za kuwapo kwa matabaka ya watu nchini na haikubaliki.
Hatukutaja, makusudi, ukumbi ambapo uzinduzi wa Chozi la Sitti
utafanyika lakini tuna hakika, Nipashe, polisi ina intelejensia ya
kutosha kuufahamu kirahisi.
Sitti Mtemvu akamatwe.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment