Siku tatu baada ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi
yaendayo mikoani (Taboa), kuendelea na msimamo wa kugoma nchi nzima
kupinga nauli mpya, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra), imenywea na kufuta agizo lake la awali la kupunguza
nauli hizo.
Badala yake, Sumatra imetangaza kusitishwa utekelezaji wa viwango
vipya vya nauli vilivyotangazwa hivi karibuni na kutaka vya zamani
viendelee.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sumatra kwa vyombo vya habari,
jana jijini Dar es Salaam, na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Gilliard
Ngewe, utekelezaji utasitishwa hadi marejeo yatakapofanyika tena.
“Sumatra imepokea kutoka kwa msafirishaji ABC Trans na Afritrans
Limited maombi ya kupitia upya maamuzi yake ya kushusha viwango vya
nauli za mabasi ya masafa marefu yalitolewa kwa Agizo Na. SMTRA/02/2015
la Aprili 15, mwaka huu. Maombi ya Kampuni mbili yalipokelewa Sumatra
Aprili 29, mwaka huu, kwa mujibu wa Kifungu Na 19 (2)(b) cha Kanuni za
Tozo za mwaka 2009,” alisema.
Alisema kwa sasa viwango vya nauli vya zamani vitaendelea kutumika hadi hapo umma utakapotaarifiwa vinginevyo.
Afisa Uhusiano wa Sumatra, David Mziray, alisema sheria inatoa haki
kwa wahusika kukata rufaa ndani ya siku 14 na kwamba kwa sasa wanapitia
hoja zao kuona kama zina mashiko ndipo watatoa maamuzi ambayo yatawekwa
wazi.
Alisema viwango vipya vya nauli vilitolewa baada ya kukokotoa na
kwamba kwa mujibu wa kanuni na kwamba mambo yatawekwa wazi ndani ya siku
14.
Aprili 15, mwaka huu, Sumatra ilitangaza viwango vipya vya nauli
ambavyo vilipaswa kuanza kutekelezwa jana, kwa kupandisha nauli za
mabasi huku za usafiri wa mijini ukibaki kama ulivyo.
Aprili 27, mwaka huu, Taboa ilitangaza mgomo nchi nzima kupinga maamuzi ya Sumatra ya nauli mpya.
Post a Comment