Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Wizara ya Ujenzi kutoa majibu ya
deni la zaidi ya Sh. bilioni 800 inayodaiwa wizara hiyo na makandarasi
katika bajeti ya mwaka 2014/2015.
Akiwasilisa hotuba ya Kambi hiyo kuhusu Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Msemaji Mkuu wa Kambi
hiyo, Felix Mkosamali, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014,
wizara hiyo ilitengewa Sh. 662,234,027,000 kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Januari 2014, madeni ya
makandarasi na washauri yalikuwa Sh. 663,870,636.26.
Alisema mfano mzuri ni bajeti 2014/2015 wizara ilikuwa na madeni
yaliyofikia Sh. bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na
taasisi zake ikiwa ni Sh. bilioni 762.
“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inamtaka waziri kueleza ukweli
Bunge lako tukufu kwamba kwenye bajeti ya 2014/2015 ni fedha kiasi gani
zimelipa madeni na fedha kiasi gani zimekwenda kwenye miradi ya
maendeleo,” alisema.
Mkosamali alisema hata kwa mwaka huu wa fedha, Bajeti ya Maendeleo
ni Sh. 890,572,000.00 kwa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara huku
madeni yakiwa zaidi ya Sh. bilioni 800. “Hakuna uhalisia kati ya fedha
za maendeleo zinazoombwa na madeni husika.”
Alisema wizara hiyo imekuwa kiandika hotuba ndefu kuwachanganya
wabunge kwa kuonyesha barabara zilizojengwa miaka ya 80 na miaka 90 kama
vile zimejengwa hivi karibuni.
Alisema wizara haijatoa ufafanuzi unaoridhisha juu ya fedha
zinazotengwa na kilomita zinazojengwa, mfano wa Barabara ya Dar es
Salaam – Chalinze – Morogoro (kilomita 200), sehemu ya Dar es Salaam
Chalinze imetengewa Sh. bilioni 2.45. “Hakuna ufafanuzi kwani kilomita
100 haziwezi kujengwa kwa Sh. bilioni mbili tu.”
MADARAJA YALIYOAHIDIWA
Kambi hiyo ilisema licha ya mbwembwe nyingi za waziri, madaraja
yaliyoahidiwa kujengwa mwaka 2014/15 likiwamo la mto Sibiti
lililotengewa Sh. bilioni tatu, lakini fedha hizo hazijatolewa na Hazina
na mkandarasi ameondoka eneo la ujenzi na Daraja la Kigamboni ambalo
liliahidiwa kukamilika mwezi Juni, mwaka huu, ambalo linaonyesha ahadi
haitatekelezeka.
BARABARA CHINI YA KIWANGO
Kambi hiyo ilisema licha ya wizara na hata Waziri Mkuu kujigamba
kujenga kilomita 13,000 za lami katika awamu ya nne, zimejengwa chini ya
kiwango na zinabomoka na kuharibika miezi sita au pungufu au mwaka
mmoja baada ya matengenezo.
Alitoa mifano hiyo kuwa ni Dar es Salaam – Dodoma ambayo imebonyea
upande wa kushoto na inatengenezwa kila wakati, lakini inaharibika,
Bagamoyo – Msata, ambayo imeanza kuharibika kabla haijamalizika, Dodoma –
Iringa, imejaa mashimo maeneo kadhaa na Dodoma – Mwanza hasa maeneo ya m
lima wa Sekenke iliyobomoka muda mfupi mara tu ya kukabidhiwa
serikalini.
UNUNUZI KIVUKO DSM-BAGAMOYO
Kambi hiyo ilikiponda kivuko hicho chenye kubeba abiria 300 kwa
karibu Sh. bilioni nane, lakini kinatumia saa tatu kutoka Dar es Salaam
hadi Bagamoyo.
“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani chenye spidi ndogo.
Azam Bakhresa ana meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika
90 tu na kinabeba abiria 500, ambacho kwa taarifa tulizonazo
kimemununuliwa kwa kati ya Sh. bilioni nne hadi tano tu,” alisema.
KUPUNGUZA MSONGAMANO DAR
Kambi hiyo ilisema inaamini juu ya ujenzi wa barabara zipitazo juu
ili kuepusha kero kwenye maeneo ya Tazara, Moroco, Ubungo, Magomeni,
Selander bridge na maeneo mengine yenye msongamano.
Hata hivyo, ilisema serikali haina nia ya dhati ya kuonyesha msongamano huo kwa kujenga angalau barabara moja inayopita juu.
BARABARA ZISIZOTEKELEZWA AHADI
Mkosamali alisema licha ya mbwembwe za uwasilishaji wa waziri wa
bajeti hiyo, kila inapofikia mwaka wa uchaguzi, serikali imekuwa
ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura, lakini haitimizi
ujenzi wa barabara hizo.
Alitaja barabara hizo kuwa ni ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu,
Kidahwe zenye urefu wa kilomita 310 ambayo ilikuwa ahadi ya Serikaliya
awamu ya tatu na awamu ya nne.
Barabara nyingine ni Karatu – Mang’ola –Matala, ambayo iliahidiwa
kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa haijajengwa pamoja na
ahadi yake kutolewa mwaka 2010 na wananchi kuendelea kula vumbi.
Alitaja barabara nyingine kuwa ni Karatu – Mbulu (Kilomita 77),
Arusha – Moshi – Himo –Holili (kilomita 140), Bunda – Kisorya –Nansio
(kilomita 93) na Kilombero – Ifakara – Mahenge.
Nyingine ni Mpemba – Isongole (kilomita 51.5), Kalando- Meatu –Mto
Sibiti –Singida na barabara za miji midogo ambazo zilitolewa ahadi ya
ujenzi na Rais wa awamu ya nne za mji wa Karatu (kilomita 2), Kibondo
Mjii (kilomita 1.5) na ujenzi wa lami Kondoa.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق