Dodoma. Mjadala wa bajeti mwaka 2015/16
umegeuka mwiba mchungu kwa Ofisi ya Rais baada ya mawaziri watatu
waliopo katika ofisi hiyo kubanwa na wabunge wa upinzani hasa wale
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakisema “njaa imeanzia
Ikulu na Ofisi ya Rais inayosimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) haina utashi wa kupambana na rushwa.”
Mawaziri hao jana walitakiwa kueleza sababu za
ofisi hiyo kushindwa kutokomeza rushwa, mikakati ya Serikali kuiwezesha
Takukuru na kuipa meno ya kuwashtaki moja kwa moja watuhumiwa wa rushwa.
Kambi hiyo imeilipua Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete
wakitaka ifutwe kwa maelezo kuwa imekiuka sheria za nchi.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Muhambwe
(NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliibua malumbano makali kati yake na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na
Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, baada ya kudai kuwa Ikulu na
Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kupambana na rushwa licha ya kuwa
chini ya Rais.
Alivyochafua hali ya hewa
Katika mjadala huo, Mkosamali alihoji; “kama
Takukuru, Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) ziko
chini ya Ofisi ya Rais na bado zinalia njaa, kwa nini watumishi wa umma
kama wauguzi na walimu wawe chini ya ofisi hii badala ya kuwa katika
Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi?
“Yaani njaa imeanzia Ikulu. Tumeiweka Takukuru
Ikulu tukidhani kuwa Rais ataweza kupambana na rushwa, sasa ukiona
taasisi hiyo imefeli tambua kuwa Rais hana utashi wa kisiasa wa
kupambana na rushwa
“Watu wanajua Takukuru ikiwatuhumu katika kesi
kubwa zitafutwa. Taasisi hii kufeli kufanya kazi maana yake ni kuwa
Serikali imefeli katika miaka yote minane, hata Rais hakuwa na nia ya
kupambana na rushwa,” alisema na kusisitiza jinsi Bunge la Katiba
lilivyoshindwa kuipa meno Takukuru kupitia Katiba Inayopendekezwa.
Alihoji, “Tasaf wameomba Sh18 bilioni mwaka jana
na mpaka sasa wamepewa Sh3 bilioni na sasa hivi mnaomba tena mabilioni
ya shilingi. Hivi mnataka wakurugenzi wa Tasaf na wafanyakazi
wawachukuliaje?”
Alihoji taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais
kutopewa fedha za bajeti kama ilivyoidhinishwa mwaka jana na kusema
kitendo cha mwaka huu wizara tatu za Ofisi ya Rais kuja na bajeti
nyingine wakiomba mabilioni ya fedha ni fedheha.
“Kama taasisi zilizopo Ikulu zina njaa, hivi
nyinyi huko katika halmashauri si ndiyo mtakufa! Rais ambaye taasisi
hizi zipo ofisini kwake anashindwa kuzihudumia atawakumbuka watu wa
Kibondo? Hii Serikali imechoka kabisa na imechakaa,” alisema.
Kauli hiyo ilimnyanyua Mkuchika na kuomba kutoa
taarifa, jambo ambalo lilipingwa na Mkosamali akidai kuwa awali aliomba
kutoa taarifa kwa mwenyekiti na kunyimwa
- Mwananchi
Post a Comment