Wabunge wa Ukawa waikalia kooni Ikulu

Dodoma. Mjadala wa bajeti mwaka 2015/16 umegeuka mwiba mchungu kwa Ofisi ya Rais baada ya mawaziri watatu waliopo katika ofisi hiyo kubanwa na wabunge wa upinzani hasa wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakisema “njaa imeanzia Ikulu na Ofisi ya Rais inayosimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haina utashi wa kupambana na rushwa.”
Mawaziri hao jana walitakiwa kueleza sababu za ofisi hiyo kushindwa kutokomeza rushwa, mikakati ya Serikali kuiwezesha Takukuru na kuipa meno ya kuwashtaki moja kwa moja watuhumiwa wa rushwa.
Kambi hiyo imeilipua Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete wakitaka ifutwe kwa maelezo kuwa imekiuka sheria za nchi.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliibua malumbano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, baada ya kudai kuwa Ikulu na Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kupambana na rushwa licha ya kuwa chini ya Rais.
Alivyochafua hali ya hewa
Katika mjadala huo, Mkosamali alihoji; “kama Takukuru, Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) ziko chini ya Ofisi ya Rais na bado zinalia njaa, kwa nini watumishi wa umma kama wauguzi na walimu wawe chini ya ofisi hii badala ya kuwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi?
“Yaani njaa imeanzia Ikulu. Tumeiweka Takukuru Ikulu tukidhani kuwa Rais ataweza kupambana na rushwa, sasa ukiona taasisi hiyo imefeli tambua kuwa Rais hana utashi wa kisiasa wa kupambana na rushwa
“Watu wanajua Takukuru ikiwatuhumu katika kesi kubwa zitafutwa. Taasisi hii kufeli kufanya kazi maana yake ni kuwa Serikali imefeli katika miaka yote minane, hata Rais hakuwa na nia ya kupambana na rushwa,” alisema na kusisitiza jinsi Bunge la Katiba lilivyoshindwa kuipa meno Takukuru kupitia Katiba Inayopendekezwa.
Alihoji, “Tasaf wameomba Sh18 bilioni mwaka jana na mpaka sasa wamepewa Sh3 bilioni na sasa hivi mnaomba tena mabilioni ya shilingi. Hivi mnataka wakurugenzi wa Tasaf na wafanyakazi wawachukuliaje?”
Alihoji taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais kutopewa fedha za bajeti kama ilivyoidhinishwa mwaka jana na kusema kitendo cha mwaka huu wizara tatu za Ofisi ya Rais kuja na bajeti nyingine wakiomba mabilioni ya fedha ni fedheha.
“Kama taasisi zilizopo Ikulu zina njaa, hivi nyinyi huko katika halmashauri si ndiyo mtakufa! Rais ambaye taasisi hizi zipo ofisini kwake anashindwa kuzihudumia atawakumbuka watu wa Kibondo? Hii Serikali imechoka kabisa na imechakaa,” alisema.
Kauli hiyo ilimnyanyua Mkuchika na kuomba kutoa taarifa, jambo ambalo lilipingwa na Mkosamali akidai kuwa awali aliomba kutoa taarifa kwa mwenyekiti na kunyimwa
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم