Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
imewaona wafanyakazi wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanaokabiliwa
na tuhuma za kughushi vyeti na kutoa hati za uongo wana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi,
Nyigulile Mwaseba baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi
wanane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa
mahakamani hapo.
Baada ya Hakimu Mwaseba kutoa uamuzi huo, alisema
Juni 17 na 18, 2015, washtakiwa hao ambao wanadaiwa kuwa ni watoto wa
vigogo wa Serikali wataanza kutoa ushahidi wa utetezi dhidi ya mashtaka
yanayowakabili.
Wafanyakazi hao ni Justina Mungai, Christina
Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beatha Massawe, Jacquiline
Juma, Philimina Mutagurwa na Amina Mwinchumu.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao, BoT.
Washtakiwa Mungai, Massawe na Mwinchumu, wanadaiwa
kughushi vyeti hivyo mwaka 2001, wakati Ntemi, Kombakono, Mahenge na
Mutagurwa wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002.
Wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha
nne na kutoa BoT hati za uongo wakionyesha kuwa vimetolewa na Baraza la
Mitihani la Taifa wakati siyo kweli. Washtakiwa hao ambao awali
waliyakana mashtaka, wako nje kwa dhamana.
إرسال تعليق