Waziri afunguka kuporomoka kwa shilingi

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, amesema Tanzania inahitaji kuimarisha viwanda vyake vya ndani kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa viwango vya kimataifa ili kuirudisha shilingi kwenye thamani yake.
Shilingi ya Tanzania imeporomoka kwa asilimia 21 ambapo moja ya sababu ni kushuka kwa mauzo ya bidhaa za ndani, nje ya nchi. Dola moja ya Marekani kwa sasa inabadilishwa kwa Shilingi 2000 ya Tanzania.

NIPASHE Jumapili katika mahojiano na Dk. Kigoda, kuhusu mikakati ya serikali ya kuinusuru shilingi ya Tanzania isiendelee kuporomoka, alisema tatizo lililopo ni nchi kukosa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazofanya vizuri soko la nje.

Alisema ili nchi ifanye vizuri kwenye soko la nje yapo masharti kadhaa ambayo yanatakiwa kufikiwa ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji ndani na nje.

Alisema lazima nchi iiangalie mifumo yake ili mwekezaji anapotaka kuwekeza kwenye ardhi aipate kwa muda muafaka bila ya kuwa na milolongo mirefu na kuwapo kwa uhakika wa nishati ya umeme wakati wote.

“Tunaona serikali sasa imejitahidi kwenye hili kuhakikisha nishati ya umeme hapo baadaye inakuwa yenye ubora na sio ya kusuasua,” alisema na kuongeza:

“Wawekezaji wengine wanapoona gharama za umeme zipo juu wanaona ni bora waagize bidhaa nje ya nchi na kuziuza ndani, badala ya kuzizalisha kwenye viwanda vyao hapa,” alisema.

Aidha, kuhakikisha kunakuwapo na mpangilio wa kodi, vigezo ambavyo wawekezaji huangalia wanapotaka kuwekeza.

Serikali pia inatakiwa kuongeza msisitizo wa viwanda vidogo na vya kati kuzalisha bidhaa zenye ubora na kiwango.

Katika ushindani, alisema lazima nchi ifikie mahali ihamasishe uzalishaji bidhaa zenye kiwango.

“Wapo Watanzania ambao wanauza bidhaa zao Marekani, Uingereza lakini bado hawapo kwenye ushindani mkubwa,” alisema.

Alitaja aina za bidhaa zinazouzika kwenye masoko ya nje kuwa ni nguo zinazotengeneza hapa nchini, kahawa, mboga na matunda.

Hata hivyo, alisema bado wanatakiwa kubuni vitu mbali mbali vitakavyopata soko la nje.

Mchumi na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Donath Olomi, alisema mahitaji ya dola yanachangiwa na biashara ya ndani kuendeshwa kwa dola.

“Mfano ni kwenye mahoteli au majengo ya kukodi unakuta huduma zake zinachajiwa kwa dola wakati vipo vitu ambavyo havihitaji kulipwa kwa dola, hili linachangia dola kupanda,” alisema na kuongeza:

“Kwingineko duniani nchi husika inapaswa kununua kwa fedha ya nchi husika badala ya dola na hii husaidia thamani ya fedha ya nchi husika kupanda,” alisema.

Aidha, alisema kuporomoka kwa shilingi siyo tatizo la Tanzania peke yake, bali fedha nyingi za nchi  zimekumbwa na adha hiyo kutokana na kupanda kwa dola.

Alisema tatizo hilo limetokana na thamani ya dola kupanda kwa kuwa uchumi wa Marekani umeimarika kwa siku za hivi karibuni.

Dk. Ulomi alisema inapotokea mahitaji yakapanda ghafla kawaida bei nazo hupanda.

“Kwa sasa mahitaji ya dola ni makubwa kuliko upatikanaji wake, dola tunazipata kupitia bidhaa tunazoziuza nje, mikopo, kusimamishwa kwa misaada ya wafadhili mwaka uliopita kulisababisha kushuka kwa dola,” alisema.

Aliongeza kuwa inawezekana kushuka kwa shilingi kunatokana na wafadhili kuzuia misaada yao

Post a Comment

Previous Post Next Post