Mabehewa feki 47 yatua kimya kimya

Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta
Agizo la serikali la kupiga marufuku uingizaji wa mabehewa ‘feki’ ili kuliokoa taifa dhidi ya ufisadi na ajali zinazogharimu mali na maisha ya watu, limepuuzwa baada ya Kampuni ya Reli (TRL) kupokea mabehewa 47, mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Mabehewa hayo ni sehemu ya yaliyoanza kuingizwa nchini, Julai 24, mwaka jana na kupokelewa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Hata hivyo, serikali kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, ilizuia uingizwaji wake, Aprili 16, mwaka huu, kwa madai kuwa hayana ubora.

Akitangaza uamuzi wa kuzuia mabehewa hayo, Sitta alisema baada ya bodi kupitia taarifa hiyo, ilibaini  mabehewa mengi kati yaliyoagizwa yalikuwa na kasoro, kuwepo kwa uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kuanzia kiwandani  na kuwapo kwa uzembe katika mchakato wa kuyapokea.

Sitta alisema kilichowashtua ni kubaini ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi ambao ulipangwa kufanyika kwa awamu.

Alisema katika makubaliano ya ununuzi wa mabehewa hayo, malipo yalitakiwa yafanywe kwa awamu kwa kuanza na asimilia 50 awamu ya kwanza,  asilimia 40 awamu ya pili  na awamu ya mwisho ya malipo ilikuwa ni asilimia 10.

Hata hivyo, wiki mbili tangu Sitta atoe agizo hilo, gazeti hili limebaini kuwa mabehewa 47 yaliingizwa nchini na kuhifadhiwa kwenye karakana ya Malindi jijini Dar es Salaam.

Chanzo chetu cha habari kiliiambia NIPASHE Jumapili mabehewa hayo yameingia mwanzoni mwa wiki iliyopita na kupokelewa kimya kimya bandarini bila viongozi kuwapo.

Chanzo hicho kimesema inavyoonyesha mkataba wa kuyaleta mabehewa hayo haujavunjwa ndio maana yamewasili tena licha ya Waziri Sitta kusema yaliyobaki yasiingie nchini.

NIPASHE ilishuhudia mabehewa hayo yakiwa kwenye karakana hiyo yakiwa yameandikwa: "Manufactured by Hindustthan Engineering and Industries LTD. Kalkata, India 2014:"

Mabehewa hayo ni kati ya 274, ambapo 150 yalishaingizwa nchini na mengine 124 yalizuiliwa.

Sakata la ununuzi wa mabehewa hayo limesababisha serikali hasara ya Sh. bilioni 230. Kufuatia sakata hilo Sitta aliwasimamisha kazi vigogo watano kutokana na kubainika kuihujumu serikali.

Waliosimamishwa ni Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu,  Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi Fedinarnd Soka.

Post a Comment

Previous Post Next Post