Kama umeumbwa na moyo wa kibanadamu na ukapata nafasi ya kuona
kile alichokiandika msanii maarufu, Wema Sepetu kuhusu suala lake la
kutoweza kupata ujauzito basi ni wazi kwamba ulihuzunika sana.
Hata mimi pia nilihuzinika, lakini nilihisi vibaya
zaidi nilipokumbana na maneno yasiyo ya kiungwana yaliyoongelewa kwenye
mitandao kumhusu Wema.
Hivi karibuni mwanadada huyo aliyewahi kuwa Miss
Tanzania, aliandika katika ukurasa wake wa instagram kuwa hana uwezo wa
kupata mtoto.
Ingawa Wema ambaye alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platinum hakuweka
wazi ni tatizo lipi linalomsibu lakini ukisoma ujumbe huo utagundua
kuwa mwanadada huyo huenda amepata taarifa za kitabibu kuwa hawezi
kupata mtoto tena katika kipindi cha maisha yake.
Kutokana na waraka huo, wapo waliomuonea huruma na
kumpa pole kutokana na tatizo hilo, lakini pia wapo waliomkejeli na
kumwambia kwamba hayo ni matokeo ya matendo yake ingawa sina uhakika
kama watu hao wana uthibitisho wa waliyokuwa wakiyasema, ila kwasababu
mitandao ya kijamii inatoa uhuru wa kuzungumza chochote unachojisikia,
hata kama ni kibaya watu wanaandika kile kinachokuja katika vichwa vyao.
Lakini nikigeukia kwa Wema, napata maswali mengi
sana. Najiuliza alitafakari mara ngapi kabla ya kutenda haya? Aliwaza
nini hadi kuandika ujumbe wa namna ile? Je alifikiria athari zake?
Sote tunajua mitandao ya kijamii hivi sasa inavyotumika vibaya. Je, Wema alizingatia hilo?
Wapo mabingwa wanaosifika kwa tabia za kuwachafua
wenzao kwa kutumia mitandao ya jamii. Baadhi ya watu sasa wanashinda
kutwa kucha mitandaoni kwa lengo la kuharibu heshima za wengine. Je,
hili nalo Wema alikuwa akilijua kabla ya kufanya uamuzi wake?
Bila shaka lengo lake lilikuwa ni kuwafahamisha
wale wote wanaomsema vibaya kwamba hana mtoto kwa sababu anaendekeza
ujana, lakini binafsi nahisi amefeli na laiti kama ningekuwa mtu wake wa
karibu ningemshauri asiandike kwa mtindo ule alioutumia.
Naamini sasa ujumbe ule umemsababishia maumivu
zaidi ya yale aliyokuwa nayo kabla ya kuandika kwani wengi walitoa maoni
ya kumkashifu.
Wema alitakiwa kufahamu kwamba shabiki si ndugu
yake, ni mteja wa bidhaa anayoiuza tu, iwe ni filamu au vingine vyote
anavyofanya. Kwa uhalisia sidhani kama muuza genge mwenye tatizo la
kufanana na hilo atakuwa akimueleza kila mteja wake anayekuja gengeni
kwake kununua nyanya na vitunguu.
Pia ni lazima aelewe kuwa si yeye pekee mwenye
tatizo hilo. Kuna familia nyingi huku mtaani zinahangaika kupata mtoto
mchana na usiku. Lakini waathirika wa tatizo hilo hawathubutu kusimama
hadharani na kutangaza tatizo lao ingawa jamii inayowazunguka imekuwa
ikiwajadili kila kukicha.
Post a Comment