London, Uingereza. Kwa mara nyingine, Jina la nchi limeendelea
kuchafuka baada ya Meli ya MV Hamal iliyosajiliwa Tanzania kukamatwa
barani Ulaya ikiwa imebeba shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine
yenye uzito wa tani tatu.
Kama dawa hizo haramu zingeuzwa mitaani nchini
Uingereza, zingekuwa na thamani ya Sh1.5 trilioni, kiasi ambacho nchi
wafadhili zinatarajiwa kuichangia Tanzania kwenye bajeti ya mwaka
2015/16.
Matukio mengine yaliyoichagua nchi ni la meli ya
mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa Septemba
2013, jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini
Italia wakati ikielekea Uturuki ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya
aina ya bangi zenye thamani ya Pauni 50 milioni za Uingereza (sawa na
Sh125 bilioni). Tukio jingine ni lile la Watanzania wawili kukamatwa na
dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye
Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Kiwango hicho cha dawa zilizokamatwa kimeweka
rekodi ya ukubwa wa mzigo wa dawa hizo haramu nchini Uingereza. Awali
shehena ya cocaine iliyokuwa kubwa ilikamatwa Septemba mwaka jana ikiwa
na mzigo wenye thamani ya Sh450 bilioni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza,
meli ya MV Hamal ilikamatwa kwenye Bahari ya Kaskazini na baada ya
kupekuliwa kwenye bandari ya Arberdeen nchini Scotland, ilikutwa na
shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 32 na uwezo wa
kubeba tani 422, ilikamatwa na askari wa kikosi cha majini cha Royal
Navy waliokuwa kwenye meli ya HMS Somerset pamoja na askari wa uhamiaji
wa Border Force waliokuwa kwenye meli ya Valiant, karibu kilomita 160
mashariki mwa mji wa Aberdeen Alhamisi baada ya kupewa taarifa na
kitengo cha makosa ya jinai, NCA.
Baadaye, meli hiyo ilipelekwa bandari ya Aberdeen,
ambako maofisa wa Border Force wenye stadi maalumu ya upekuzi,
waliipekua meli hiyo kwa kusaidiana na polisi wa Scotland.
John McGowan – afisa mwandamizi wa uchunguzi wa
NCA, alisema: “Upekuzi wa meli ulikuwa mrefu na unaosababisha maumivu,
na uliofanywa na watu wenye utalaamu mkubwa wa kufanya kazi kwenye
mazingira magumu.
“Matokeo yake ni ugunduzi huu mkubwa – unaoaminika
kuwa mkubwa kuwahi kutokea kwenye rekodi nchini Uingereza na ambao
unaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya fedha.”
Hata hivyo, rekodi za mtandao wa shughuli za
baharini unaonyesha kuwa katikati ya Februari, meli hiyo ilikuwa Uturuki
na wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife
nchini Hispania na ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili
kwa ukubwa nchini Ujerumani ikitazamiwa kufika jana usiku.
Meli hiyo imekutwa na watu tisa wenye umri kati ya
miaka 26 na 63 wote raia wa Uturuki na wameshitakiwa kwa kukutwa na
dawa za kulevya. Washitakiwa wote hawakusema lolote waliposomewa
mashtaka yao. Washitakiwa hao ni Mustafa Ceviz, 54, Ibrahim Dag, 47,
Mumin Sahin, 45, Muhammet Seckin, 26, Umit Colakel, 38, Kayacan
Dalgakiran, 63 na Emin Ozmen, 50, wote wanatoka jiji la Istanbul.
Wengine ni Abdulkadir Cirik, 31, anayetoka Mersin na Mustafa Guven, 47,
kutoka Yozgat, nchini Uturuki. Walifikishwa mahakamani Jumatatu.
Balozi wa Tanzania azungumza
Post a Comment