Straika Man U asubiriwa Azam

AZAM hawataki mchezo, wameamua kufanya kweli kwa kuanza mchakato wa kumleta straika wa zamani wa West Ham Utd aliyewahi kukuzwa katika klabu ya Man United, Joe Dixon ili imsajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Muingereza huyo aliyekuwa akiichezea Fenerbahce ya Uturuki aliwahi kufanya mazoezi timu ya vijana ya Man Utd na wakali kama Danny Welbeck na anatarajiwa kutua siku yoyote kuanzia leo ili asaini mkataba wa kuichezea Azam baada ya kocha Stewart Hall kumpendekeza.
Dixon, 26, ambaye Novemba mwaka jana alitajwa kama mchezaji mwenye kasi akiwashinda hata Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Theo Walcot na Lionel Messi atachuana na Jimmy Ndlovu anayekipiga Power Dynamos ya Zambia kuwania nafasi ya kusajiliwa Azam.
Stewart alisema, nafasi mbili za wachezaji wa kigeni ni kipa na straika mwenye akili, kasi na uwezo wa kucheza namba zote za mbele, si tisa tu, yaani 10, 11 na 7.
“Tumezungumza na straika Muingereza atakuja muda wowote wiki hii na kila kitu kinakwenda sawa.”
“Atakapokuja atafanya mazoezi kila mtu amwone, sina wasiwasi naye,” alisema na kufafanua, kati ya Dixon na Ndlovu atakayekuwa vizuri zaidi atasajiliwa.
“Nataka straika lakini asiwe anajua kucheza namba tisa pekee, awe na uwezo wa kucheza nafasi zote za juu) kwa sababu washambuliaji wa hivyo ninao wengi,” alisema akiwatolea mfano Ame Ali, John Bocco, Tchetche na Kavumbagu.

Post a Comment

Previous Post Next Post