Uongozi Simba usipojipanga kocha atakwama

JANA Jumatatu klabu ya soka ya Simba ilimtangaza kocha mpya, Muingereza, Dylan Kerr anayechukua nafasi ya Goran Kopunovic aliyeshindwa kuelewana na uongozi wa timu hiyo katika suala la maslahi.
Kwa Afrika Mashariki, Kerr ni jina geni lakini katika kazi ya ukocha si jina geni kwani amewahi kuifanya kazi hiyo katika klabu mbalimbali nchini Afrika Kusini pamoja na Vietnam.
Sambamba na kuifanya kazi hiyo, Kerr pia ni mtaalamu wa viungo kama alivyokuwa msaidizi wa zamani wa kocha wa Stars, Itamar Amorin ambaye baadaye alikuwa kocha mkuu wa klabu ya Azam.
Kerr pia amewahi kucheza soka la kiwango cha juu akiwa beki wa kushoto akizichezea klabu zilizowahi kutamba kwenye Ligi Kuu England za Sheffield Wednesday, Leeds United na Reading.
Ukiachana na historia yake na kuizungumzia kazi yake mpya ya kuinoa Simba, Kerr ni mgeni kwa maana ya kwamba hana uzoefu sana na nafasi ya ukocha mkuu.
Katika timu nyingi alizowahi kuzifundisha rekodi zinaonyesha kwamba ni timu moja tu ambayo alikuwa kocha mkuu, Hi Phòng ya Vietnam aliyoanza kuinoa akiwa msaidizi kabla ya kuwa kocha mkuu na kuiwezesha kutwaa taji la Vietnam. Hatusemi kwamba sifa zake zinamuondolea heshima ya kuwa kocha wa Simba, tunaamini uzoefu alionao unatosha kuinoa timu hiyo.
Tunachotaka kusisitiza hapa ni kwa viongozi Simba kujipanga ili kuhakikisha kocha wao mpya anafanya kazi yake kwa amani ili atakapoharibu waweze kumbana.
Tunasema hivyo kwa sababu kama tulivyosema awali Kerr ni mgeni na soka la Tanzania, na zaidi ya hilo hatutarajii ashiriki kikamilifu kwenye usajili wa wachezaji, atakabidhiwa Simba iliyoandaliwa na watu wengine. Kwa muda ambao ataanza kufanya kazi viongozi wa Simba wajipange kuhakikisha matatizo madogo madogo hayapewi nafasi ya kuvuruga mipango yake. Kwa mfano kuna wakati kiungo wa Simba, Hassan Kessy alisusa kuichezea Simba wakati ligi ikiendelea kwa sababu uongozi ulikuwa haujamtimizia ahadi zake.
Haya ni kati ya mambo ambayo tusingependa yaibuke wakati kocha wa Simba akianza kazi.
Kwa mantiki hiyo viongozi wa Simba ambao wanaendelea na harakati za usajili wa wachezaji waliangilie hilo kwa umakini wa hali ya juu. Usajili wa aina yoyote ni lazima uzingatie uwezo wa klabu na viongozi wajipange kuhakikisha ahadi wanazowapa wachezaji zinaheshimiwa kwa wakati.
Kutoheshimu ahadi za wakati wa kuwasajili wachezaji inaweza kuwa sababu ya Kerr naye kuonekana hafai na kutimuliwa au kuondoka mwenyewe. Ni vyema wachezaji ambao kocha atawakuta na kufanya nao mazoezi awe na uhakika wa kuwatumia mwanzo hadi mwisho wa msimu ili kazi yake iwe rahisi.

Post a Comment

Previous Post Next Post