Dar es Salaam. Mwanamuziki wa
kizazi kipya Diamond Platnum, ameeleza kushangazwa kwake na ukimya wa
Serikali akisema unaashiria kutotambua tuzo ya kimataifa aliyoipata hivi
karibuni kupitia MTV.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
jana, nyota huyo alidai kuwa hali hiyo inachangia kuwakatisha tamaa
wasanii, huku Baraza la Sanaa la Taifa, (Basata) likieleza kuwa haikuwa
na taarifa za siku rasmi ya kurejea Diamond ndiyo sababu wameshindwa
kushiriki.
Diamond anayetamba na wimbo wa Nana, wiki
iliyopita alinyakua Tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Afrika mjini Durban,
Afrika Kusini na ambayo ilishindaniwa pia na Mr Flavor wa Nigeria,
Micassa wa Afrika Kusini, To Fun wa Togo na Big Nuz wa Afrika Kusini.
Alisema
kuwa licha ya Watanzania wengi kumpongeza kwa mafanikio hayo, hakuna
kiongozi wala taasisi ya Serikali iliyozungumza chochote kuhusu ushindi
huo uliopatikana kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.
“Nilitarajia
taasisi za Serikali zinazohusika na sanaa, zingekuwa mstari wa mbele
kuonyesha furaha kutokana na mafanikio haya, lakini mpaka leo hakuna
niliyemsikia akizungumzia, wakati ni tuzo kubwa na imeleta heshima kubwa
kwa Watanzania,”alisema Diamond.
Kwa upande wake,
Meneja wa Msanii huyo Salam Sharaf alisema wakati umefika wa Serikali
kugeukia nyanja zingine za burudani badala ya kuweka mkazo kwenye mpira
pekee.
“Sidhani kama timu ya taifa ikishinda
watakosekana viongozi wa Serikali kwenda kuipokea, ushindi wa Diamond ni
heshima kwa taifa na taarifa zilisambaa kila kona juu ya ujio wetu,
lakini hakuna aliyetutafuta mpaka leo,”alisema.
Siku
chache baada ya kushinda tuzo hiyo jina la Diamond limeonekana kung’ara
kwenye tuzo za AFRIMMA zinazotolewa nchini Marekani akiwa ametajwa
kuwania vipengele saba.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa
Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza alisema hawakuwa na taarifa
za siku rasmi ya kurejea Diamond, ndiyo maana hawakuwepo kwenye mapokezi
yake.
“Licha ya kuwa wakati anaondoka hakusema
chochote, lakini Basata hatuna sababu ya kumtelekeza. Tungekuwa na
taarifa muda gani anawasili tungekuwepo uwanja wa ndege kumpokea, maana
ameleta heshima kubwa kwa taifa. Nampongeza sana kwa mafanikio hayo.
Tunafahamu msanii akitoka nje haendi kama mtu binafsi, bali anakwenda kuiwakilisha nchi basi tuwe tunapeana taarifa,”alisema.
Akizungumzia
tuzo za AFRIMMA juzi, Diamond alisema ataendelea kuwa mwema na kuufanya
muziki wake kama kazi kwani umetambulika kimataifa.
“Nawashukuru
kutambua kazi yangu, nadhani sasa watu watajua kwamba kuwania vipengele
hivi vyote ina maana gani,” alisema na kuongeza:
“Namshukuru
Mungu kwa kuendelea kubariki kazi yangu. Siku zote nitaendelea kuwa
mwema na kuhakikisha nafanya kazi kwa bidii kwani vipengele sita katika
tuzo za AFRIMMA si kitu kidogo.”
Wakati huohuo msanii
huyo alijibu tuhuma zinazoendelea kuenezwa dhidi yake kufuatia picha na
maelezo aliyoweka kwenye mtandao wa Instagram vinayodaiwa kumdhalilisha
mwanamitindo Jokate Mwegelo.

Picha hiyo ambayo ilikuwa
ikimuonesha Jokate akicheza wimbo wa Diamond, ilisindikizwa na maneno
“`..na bado, mtanyooka tu”, ilipokewa kwa hisia tofauti na mashabiki
pamoja na Jokate mwenyewe ambaye alimjibu nyota huyo akisema:
“Lakini
wasiwasi wangu ni kwamba huenda anafanya vile kama ilivyo kawaida yake
kudhalilisha wanawake aliotoka nao ili waonekane hawana thamani kwa
sababu hawako naye.”
Hata hivyo, Diamond alikanusha madai hayo ya udhalilishaji akisema:
“Kimsingi
sikueleweka, lengo kuu lilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa wapinzani wa
jadi, ambao kila siku wamekuwa wagumu kuuelewa muziki wangu ambao kila
kukicha unavuka mipaka. Labda kosa langu ni kutumia picha ya Jokate
ambaye mimi nilimchukulia kama shabiki, anayejulikana na wengi, ili
kufikisha ujumbe kwa urahisi.”
إرسال تعليق