Kwa Mzungu wa Simba freshi tu

WAKATI timu za Tanzania zikiwa zimezoea kucheza kwa ratiba laini ya mechi moja kwa wiki, Simba sasa inaonekana kupata kiburi baada ya kusema kuwa ratiba mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo kwa maelezo ya awali imedai kuwa kutakuwa na mechi siku za wikiendi na katikati ya wiki, kwao ni bab’kubwa na itawabeba mbele ya wapinzani wao Yanga na Azam.
Pia kocha, Dylan Kerr, ametoa mpya baada ya kusema kwamba anataka kuunda kikosi cha wachezaji 25, lakini kwenye mchezo mmoja hata akibadilisha wachezaji watano ubora uwe uleule.
Timu nyingi za hapa nchini ikiwemo Yanga na Azam mara kadhaa zimekuwa zikilalamikia ratiba ya kucheza mechi nne ndani ya wiki mbili kuwa ni ngumu jambo ambalo kocha wa Kerr amelipinga vikali akisema hilo ndiyo soka la kisasa.
TFF imesogeza mbele kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Bara hadi Septemba 12 ambapo pia miongoni mwa mikakati yao katika ratiba mpya inayofanyiwa marekebisho ni kuweka mechi kila wikiendi na katikati ya wiki.
Kerr alisema kama ratiba itakuwa hivyo itambeba kwani anatengeneza kikosi imara ambacho kitaweza kupata matokeo katika mechi za mfululizo.
Kocha huyo raia wa Uingereza alisema atatengeneza wachezaji kati ya 22 na 25 ambao watakuwa fiti kucheza wakati wowote ili ratiba hiyo isimpe shida.
“Ni uamuzi sahihi kuweka mechi mbili kwa wiki, wachezaji watakuwa imara maana kama wanacheza mara moja kwa wiki na kupumzika kwa siku nyingine saba siyo jambo zuri hasa kwa viwango vyao,” alisema.
“Kwangu nadhani itakuwa ni ratiba nzuri, nitatengeneza kikosi ambacho kitaweza kuhimili mikiki mikiki ya mechi hizo na kutupatia matokeo stahiki.
“Nataka kuwa na wachezaji kati ya 22 na 25 ambao watakuwa fiti kucheza kwa wakati wowote, hata tukifanya mabadiliko ya wachezaji wanne hadi watano katika kikosi kilichocheza mechi ya mwisho tunakuwa na uhakika wa ushindi.
“Ila sitakuwa nafanya mabadiliko bila sababu za msingi, kikosi bora ndicho kitakachocheza hata kama kilitoka kucheza siku tatu nyuma.”
Wakati huo huo kocha huyo amesema wameanza rasmi mazoezi makali ya kucheza mpira kwenye kambi yao ya visiwani Zanzibar ambapo jana Jumatano walitumia zaidi ya saa nne katika mazoezi hayo asubuhi pamoja na jioni.
Kerr alisema licha ya kwamba bado wanafanya mazoezi ya viungo na utimamu wa mwili, kambi yao ya Zanzibar imejikita zaidi katika kucheza mpira ikiwemo kuwapa wachezaji wake mbinu kadhaa za mchezo.

Post a Comment

أحدث أقدم