TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS
RELEASE)
Katibu
wa CCM Wilaya ya Mjini Ndg Mohammed Omar Nyawanga akisoma Tamko la
Mikoa Mnne ya CCM Unguja kuhusuana na Mhe Edward Lowassa. kwa Waandishi
wa habari na Makada wa CCM Afisi Kuu ya CCM Zanzibar leo.
ASALAM ALEYKUM!
Awali
ya yote, kwa niaba ya Wanachama na Makada wenzangu tuliokusanyika hapa leo,
ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Molla wetu mtukufu mwingi wa rehemu kwa
ukarimu wake na kutujaalia afya njema na uwezo wa kukutana nanyi hapa leo. Pili ninapenda kuwashukuru kwa dhati Wahariri
na Wanahabari kutoka Vyombo mbali mbali vya Habari vya hapa Zanzibar, kwa
kukubali kuitika wito wetu huu maalumu.
Sisi
tuliowaita hapa ni Wanachama na Makada wa CCM.
Baadhi yetu ni viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali za Chama, wakiwemo Wajumbe
wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya, Mikoa na Taifa. Kwa kuzingatia nasabu yetu
hio, ndio maana mkutano huu tumeamua kuufanyia katika jengo letu hili la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Lengo
kubwa la kuwaiteni hapa leo, ni kuwaelezea hisia na msimamo wetu kama wanachama
na viongozi wa CCM ambao kwa kuzingatia wajibu na majukumu tuliyonayo katika
Chama, sisi ndio wasimamizi wakuu wa Siasa, Sera na Itikadi ya CCM hapa
Zanzibar.
Hivyo
basi, kwa kuzingatia hali ya Kisiasa iliyojiri hapa nchini, tangu kumalizika
kwa Mkutano Mkuu Maalumuwa CCM wa Taifa uliofanyika tarehe 12 na 13/7/2015
mjini Dodoma, na kumchagua Mhe. Dk. John
Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kumthibitisha Mhe.
Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na uhusika wetu katika maamuzi hayo
ya Chama, tumeona ipo haja na umuhimu mkubwa wa kuitisha mkutano huu na kupitia
kwenu kuwaeleza wanachama wenzetu wa CCM na Watanzania kwa jumla, hisia na
muono wetu juu ya mustakabali wa Chama chetu na hatima ya Taifa letu.
Kama
tunavyofahamu mapema mwezi Mei 2015, Chama chetu kilitangaza ratiba ya mchakato
wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika chaguzi za Vyombo vya Dola. Ratiba hio ilihusu uteuzi wa mgombea wa kiti
cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja
na Madiwani.
Mchakato
wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar, ulianza tarehe 3/6/2015 hadi 2/7/2015, kwa
wanachama kuchukua na kuresha fomu za maombi.
Baada ya hapo vikao vya uchujaji vilianza kuanzia tarehe 4/7/2015 na
kumalizika tarehe 13/7/2015. Jumla ya
Wanachama wa CCM 42 walijitokeza kuchukua fomu za maombi na kati yao 38
walifanikiwa kukamilisha masharti yaliyotakiwa na kurejesha. Miongoni mwao walikuwemo Makamu wa Rais,
Waziri Mkuu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Majaji Wakuu Wastaafu,
Mabalozi, Mawaziri na hata wanachama wa
CCM wa kawaida tu (wakulima, wafugaji n.k).
Kwa
kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama chetu, kikao cha kwanza kabisa cha
uchujaji wa wagombea ni Kamati ya
Usalama na Maadili ya ngazi husika.
Hivyo, kwa wagombea wa Kiti cha Rais, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa
ndicho chombo cha kwanza kabisa chenye wajibu wa kuchambua kwa makini ubora wa
wanachama wanaoomba Uongozi, ama viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbali mbali
za Chama, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe
kugombea uongozi huo ama kushika nafasi zilizo kusudiwa.
Kikao
cha pili ni Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, ambayo chini ya
ibara ya 119(6)(b) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2012, imepewa
jukumu la kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya
Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu
Wanahabari!
Tumelazimika kuvinukuu vifungu hivyo
vya Katiba na Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, kwa sababu huo ndio msingi uliofuatwa na Chama chetu katika
uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume
na maelezo ya baadhi ya watu wasioitakia mema CCM na kwa kuzingatia maslahi yao
binafsi wanataka kuwaaminisha Watanzania kwamba, mchakato huo uligubikwa na
mizengwe, chuki na kila aina ya ubabaishaji, jambo ambalo sio la kweli.
Tunayasema haya sio kwa ushabiki wala
kushawishiwa na mtu au kiongozi yeyote wa CCM.
Bali ukweli ni kwamba sisi wenyewe tulikua sehemu ya mchakato huo na
tulishiriki katika kila hatua ya utekelezaji.
Na kama ni kushawishiwa basi baadhi yetu tulishawishiwa kumuunga mkono
huyo ambaye leo analalamika kuwa, CCM haikumtendea haki. Sio siri, baadhi yetu tulikubali kumsaidia na
kufanya kampeni kubwa ya kuwaomba wanachama wenzetu wa CCM wakubali kumdhamini katika Mikoa mbali mbali ya nchi yetu. Tulifanya hivyo tukifahamu vyema matakwa ya
Katiba na Kanuni za Chama chetu kwamba,
mwisho wa siku vikao halali vya Chama ndio vyenye wajibu na mamlaka ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia Katiba na
Kanuni za Chama chetu.
Hata
hivyo, wengi hapa hatujashangazwa hata kidogo na kwa kweli tulitegemea kuona
kile kilichotokea tarehe 28/7/2015 kwa ndugu
yetu Waziri Mkuu wa zamani, Kada na Kiongozi wa muda mrefu wa CCM Edward Ngoyai
Lowassa, kujitoa katika CCM na kujiunga na Chama cha upinzani cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), kwa madai kwamba, CCM imeuonea na haikumtendea haki!
Tunasema
hivyo kwa sababu tulianza kupata mashaka pale tuliposikia kauli zake wakati
akijibu maswali ya baadhi ya Waandishi wa habari kwamba, katika mchakato wa
uteuzi wa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ndani ya Chama, kwa upande wake hakuna kushindwa wala kikao chenye uwezo wa
kukata jina lake. Kimsingi, kauli hio
sio tu ni ya kukidhalilisha Chama chetu bali vile vile ni uasi! Kwani ndugu Lowassa anafahamu vyema wajibu wa
mwanaCCM na mamlaka ya kila kikao ndani ya Chama. Iweje leo atamke tena hadharani kwamba, CCM
ni lazima imteue yeye kuwa mgombea wake na hakuna mwanachama mwengine ye yotemwenye
sifawala uwezo wa kumudu kuliongoza
Taifa letu zaidi ya yeye tu peke yake!
Aidha,
ni jambo la ajabu sana kuona kuwa, wale waliokua maadui zake wakubwa
kisiasa,wakiwemo Viongozi Wakuu wa Vyama vya upinzani ambao walizunguka ndani
na nje ya nchi kulichafua jina lake na CCM, leo hii bila haya wala soni ndio
wanaosimama mbele ya Vyombo vya Habari na kupaza sauti zao eti CCM imemuonea na
kumdhalilisha Lowassa! Kama hio haitoshi,
wapo wale wanaodiriki kututisha, eti nyuma yake lipo kundi kubwa la wanaCCM
ambao wapo tayari kumfuata popote pale aendapo.
Ili
kujibu madai hayo, na kwa kupitia kwenu Waandishi wa Habari, tunapenda kutumia
fursa hii kumueleza ndugu Edward Ngonyai
Lowassa pamoja na wote wanaomuunga mkono hususan Viongozi na wanachama
wa UKAWA, kwamba:-
a)
Sisi wote tuliyopo hapa leo na maelfu
ya wanaCCM waliyo nyuma yetu hususan katika Mikoa yote ya Zanzibar, tulimuunga
mkono Lowassa katika azma yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa
Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015, sio kwa sababu ya uzuri wa suara yake au utajiri alionao hapana! Bali ni
kwa sababu ya Siasa, Sera na Ilani ya Chama alichokiamini na kukipigania, yaani
CCM. Hivyo, kwa kuwa sasa ameamua
kujitenga na CCM, basi nasi tumeamua kujitenga naye na kamwe hatuko pamoja
naye.
b)
CCM ni muumini wa Haki za Binadamu,
usawa na utawala wa sheria. Hivyo,
kujiondoa kwa Lowassa katika CCM ni sawa na ilivyokua wakati wa kujiunga
kwake. Ni suala la hiari yake na wala
hatuna ugomvi naye. Ila tunamkumbusha tu
kwamba, inawezekana kabisa umaarufu alionao sasa umejengwa kutokana na CCM, lakini
haiwezekani kabisa kuwa, umaarufu wa CCM umejengwa au kutokana na yeye. Ndio maana tunasema, Chama kwanza mtu baadae”.
c)
CCM ni Chama chenye mamilioni ya
wanachama na maelfu ya viongozi, wenye hekima, busara, mapenzi na uadilifu
mkubwa kwa wananchi. Bado kinaamiwa na kukubalika miongoni mwa wananchi wengi wa
Tanzania. Wingi huo wa wanachama wake
haitokani na wala haujaletwa na utajiri wa Viongozi wake. Bali unatokana na uimara wa Siasa, Sera na
Itikadi yake., Hivyo, hasara ya kweli
kwa CCM sio kumpoteza tajiri mmoja anaetaka kubadili Sera na Itikadi ya CCM kwa
maslahi yake binafsi na marafiki zake, bali ni kuwapoteza mamilioni ya
wanachama wake ambao wanachoshwa na viongozi walafi na wanafiki ndani ya CCM!
d)
Kwa kuzingatia ukweli huo ni wazi
kwamba, uamuzi wa Lowassa kujiondoa ndani ya CCM sio jambo la kukishtua Chama
chetu, viongozi wala wanachama wake. CCM
kamwe haiwezi kudhoofika wala kupasuka. Aidha,
hii sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na Kiongozi Mwandamizi na kujiunga
upinzani. Mwaka 1989, CCM iliwafukuza uanachama
jumla ya viongozi waandamizi 11 akiwemo Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Seif
Shariff Hamad. Akafuatia Agostino Lyatonga
Mrema, ambaye alijiunga na NCCR-Mageuzi.
Mwaka jana 2014, CCM ilimfukuza uanachama aliyekua Mwakilishi wa Jimbo la
Kiembesamaki kwa tiketi ya CCM Mansoor Yussuf Himid. Hivyo, kama wahenga walivyonena tunamuambia
Lowassa, “Kama mvuvi wa pweza tukutane
mwambani” !
e)
Tunawashangaa sana Viongozi wa baadhi
ya Vyama vya Upinzani hasa vile vinavyounda umoja wa UKAWA na hususan Viongozi
na Wanachama wa CHADEMA kwa namna wanavyoendelea kuendesha Siasa za ubabaishaji
na ulaghai kwa Watanzania. Kwa hakika ni
jambo la aibu na kufedhehesha sana kuona kwamba, hata baada kufikisha umri wa
miaka 23, tangu kuanzishwa rasmi kwa Vyama vya Upinzani hapa nchini (1992),
bado Vyama hivyo hadi leo hii vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa
kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM?Mara nyingi
tumewasikia wakijitoa kimasomaso kwakukariri nusu nusu kauli ya Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwamba, “Watanzania wanahitaji mabadiliko na
wasipoyapata ndani ya CCM watayafuata nje ya CCM”. Kwa bahati mbaya sana wasia huo wa Baba wa Taifa
unakaririwa nusu nusu.Naomba kuwakumbushaViongozi wa UKAWA kwamba, Wasia
huo wa Baba wa Taifa kwa Watanzania unaendelea kwa kutamka kwamba “Rais wa Tanzania anaweza kutoka Chama cho
chote kile, lakini Rais bora wa nchi yetu atatoka CCM!
Mwisho kabisa, ninapenda nimalizie kwa
kumpongeza sana Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuteuliwa kuwa mgombea
wa CCM wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, pamoja na wanachama wengine wote
waliojitokeza kutangaza nia hatimaye kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea
nafasi ya kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa heshima kubwa
waliyoipatia CCM na kubwa zaidi kwa kukubali kupokea bila kinyongo maamuzi ya
Chama na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanaCCM.
Post a Comment