Utafiti: Makoti ya madaktari yanahatarisha afya za wagonjwa

By Clifford Majani, Mwananchi
Historia inaonyesha kuwa madaktari walianza kuvaa makoti kama vazi la kazi takribani miaka 100 iliyopita. Kuanzia miaka ya 1800 hadi kufikia mwaka 1915 lilikuwa ni jambo la kawaida kwa daktari kuvaa koti anapowahudumia wagonjwa.
Mwanzoni madaktari walikuwa wanavaa makoti ya rangi nyeusi lakini baadaye walianza kuvaa meupe kama alama ya taaluma ya kisayansi, usafi na kuwapa matumaini wagonjwa. Madaktari wa upasuaji ndio walioanza kuvaa makoti kwa ajili ya shughuli za kitabibu.
Kama Waswahili wasemavyo, kila jambo lina faida na hasara zake. Hivi ndivyo ilivyo pia kwa makoti wanayovaa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanapowahudumia wagonjwa.
Miongoni mwa faida za makoti ya madaktari ni kwamba yana mifuko inayowasaidia kuweka vifaa muhimu vinavyohitajika wakati wa kuwahudumia wagonjwa kama vile manati ya daktari (stethoscope), kalamu na vitu vingine.
Makoti haya pia huwakinga madaktari dhidi ya hatari za kikazi hasa kurukiwa na majimaji ya mwili yatokayo kwa wagonjwa. Makoti haya pia huwa ni rahisi kuyavua kuliko nguo zingine wakati yanapochafuka kutokana na majukumu ya kidaktari. Pia makoti meupe huwapa hadhi ya kipekee na utambulisho maalumu madaktari wanapotekeleza majukumu yao ya kitaaluma. 
Katika utafiti mmoja uliochapishwa mwaka 2005 na jarida moja la maswala ya kitabibu  la American Journal of Medicine, toleo la 118, ilibainika kuwa wagonjwa wengi, asilimia 75, wanapendelea kuhudumiwa na madaktari waliovaa makoti meupe.
Makoti haya pia yalibainika kuwa yanajenga imani ya wagonjwa kwa madaktari na kusaidia wagonjwa kutumia dawa kulingana na maelekezo ya daktari. Wagonjwa pia walijengeka kisaikolojia kisaikolojia na hata kuwatambua kirahisi wanapowaona wakiingia kwenye vyumba au mazingira ya kuwahudumia.
Pamoja na faida hizo, tafiti za hivi karibuni zinabainisha kuwa makoti haya yanaweza kuwa moja ya vitu hatari vinavyosababisha athari hasi za kiafya kwa wagonjwa.
Baadhi ya wataalamu wa afya wanadai kuwa makoti meupe yanasababisha hofu kwa watoto na kwa baadhi ya wagonjwa kiasi cha kusababisha shinikizo la damu waliloliita white coat hypertension. Athari nyingine ni uwezo wa makoti haya kusambaza vimelea vya magonjwa miongoni mwa wagonjwa na jamii kwa ujumla.
Utafiti uliofanywa na Josephat A. Qaday katika Hospitali ya KCMC, Moshi hapa Tanzania na kuchapishwa mwaka 2014, ulibainisha kuwa asilimia 73.33 ya makoti ya madaktari na wahudumu wa afya, yalikuwa na bakteria wanaosababisha magonjwa.
Matokeo hayo yalifanana na yale yaliyogundulika katika utafiti uliofanyika huko Nigeria ambapo asilimia 91.3 ya makoti ya madaktari yaligundulika kuwa na vimelea hatari vya magonjwa ikiwa ni pamoja na vile vya Staphylococcus aureus ambavyo ni sugu dhidi ya dawa (MRSA).
Utafiti huo ulioongozwa na C. J. Uneke wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Ebonyi Abakaliki nchini Nigeria, ulichapishwa mwaka 2010 katika jarida la World Health and Population toleo la 11(3).
Utafiti mwingine ulioongozwa na Amy M. Treakle na kuchapishwa mwaka 2009 katika jarida liitwalo American Journal of Infection Control toleo la 37(2), nao ulithibitisha wazi kuwa makoti ya madaktari yanaweza kuwa chanzo cha kusambaza bakteria hatari kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.
Utafiti wa Burden na jopo la watafiti wenzake uliofanyika huko Uingereza na kuchapishwa mwaka 2011, nao ulibainisha kuwa makoti ya madaktari na wahudumu wa afya, yanabeba bakteria wanaosababisha magonjwa. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida liitwalo Journal of Hospital Medicine, toleo la 6(4).
Kulingana na ripoti moja ya Taasisi ya Kuzuia Magonjwa ya Taifa la Marekani (CDC), takribani watu 1.7 milioni kila mwaka huko Marekani, hupata maambukizi ya magonjwa yatokanayo na mazingira ya hospitali na watu 99,000 hufariki kutokana na maambukizi hayo.
Ripoti ya CDC inaongeza kusema kuwa takribani mgonjwa mmoja kati ya 25 wanaolazwa, hupata maambukizi kutokana na huduma za tiba wanazopewa hospitalini.
Huko nchini Canada, inakadiriwa kuwa kila mwaka maambukizi yatokanayo na mazingira ya tiba hospitalini ni kiasi cha watu 220,000 na idadi ya vifo 12,000, hutokana na maambukizi hayo.
Huko nchini India, Dk Edmond Fernandes ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Udaktari kiitwacho Yenepoya Medical College in Mangalore, anasema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa makoti ya madaktari, hasa yale yenye mikono mirefu yanasababisha maambukizi kwa wagonjwa na kuongeza gharama za tiba ambazo zingeweza kuepukwa.
“Makoti ya wahudumu wa afya yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa yanayosababishwa na bakteria hatari kama MRSA,” anasema Dk Charles P. Gerba, Profesa wa Elimu ya Vimelea vya Magonjwa katika Chuo Kikuu cha Arizona nchini Marekani.
“Wakati madaktari na wauguzi wanapogusana na vitanda vya wagonjwa wenye vimelea vya magonjwa, nguo zao zinaweza kubeba vimelea hao wa magonjwa. Vimelea hawa huendelea kuwa hai baada ya saa nyingi na kusambazwa kwa bahati mbaya miongoni mwa wagonjwa,” anaongeza Profesa Gerba.
Kutokana na ushahidi wa tafiti mbalimbali, Mamlaka ya huduma za afya ya Uingereza (The UK National Health Service) mnamo mwaka 2007, walipiga marufuku madaktari na wahudumu wa afya nchini humo kuvaa makoti meupe yenye mikono mirefu.
Hospitali nyingi nchini humo zimeanza kuwapa madaktari wake sare zenye mikono mifupi na hospitali zingine zimeanza kutumia sare zenye rangi ya blue.
Msemaji wa Shirika la West Middlesex anasema sare hizi zimeonyesha mafanikio. “Sare hizi zimeongeza mvuto wa taaluma ya madaktari.
Kiwango cha maambukizi ya MRSA (meticillin resistant Staphylococcus aureus) na Clostridium difficile yamepungua kwa miaka michache iliyopita na tunahisi kwamba, mabadiliko ya mavazi ya madaktari pamoja na mambo mengine, yamechangia kutokea kwa hali hiyo,” anaongeza msemaji huyo.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Oliver Ellis iliyochapishwa mwezi Septemba mwaka 2010 katika Jarida la BMJ Careers.
Kutokana na sababu hizi na nyingine, baadhi ya madaktari nchini Marekani wameanza kuachana na uvaaji wa makoti. Utafiti mmoja unabainisha kuwa kwa sasa ni daktari mmoja kati ya wanane anayevaa koti jeupe.
Baadhi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto na wa magonjwa ya akili, kwa muda mrefu wameachana na matumizi ya makoti haya kwa kuhisi kuwa makoti hayo yanawasababishia hofu wagonjwa wao.
Chama cha Wataalamu wa Epidemiolojia katika Huduma za Afya cha Marekani (SHEA), hivi karibuni kimetoa mapendekezo ya jinsi wahudumu wa afya wanavyoweza kupunguza maambukizi ya vimelea vya magonjwa. Mapendekezo ya SHEA yanasema kuwa madaktari wavae mavazi yenye mikono mifupi.
Kuhusu makoti meupe SHEA wanasema: “Kama makoti meupe ni lazima, madaktari wawe na makoti mengi na yanayoweza kufuliwa kila siku katika maji ya moto au kwa kutumia dawa maalumu inayoua vimelea vya magonjwa.
Pamoja na ukweli huu wa kisayansi kuwa makoti ya madaktari yanaweza kuhatarisha afya ya wagonjwa na jamii, ni muhimu kutambua kuwa haitokani na aina ya mavazi anayovaa daktari wakati wa kuhudumia wagonjwa. Hatari inatokana na mavazi hayo kutotunzwa katika hali ya usafi inayokidhi viwango vinavyopendekezwa, kutobadilishwa mara kwa mara na wakati mwingine madaktari pamoja na wahudumu wengine wa afya kuingia katika maeneo mengine nje ya hospitali kama vile katika migahawa iliyoko ndani ya hospitali, wakiwa wamevaa makoti au mavazi wanayoyatumia wakati wa kuhudumia wagonjwa wodini.
Matokeo ya tafiti hizo yanaifanya Tanzania nayo kuingia katika mpango wa kutakiwa kurekebisha kanuni ili kuepusha madaktari kuwa sababu ya wagonjwa kuambukizwa magonjwa ya ziada.
Malengo ya wagoinjwa kwenda hospitali ni kupatiwa tiba na siyo kuwa sababu ya wa kuambukizwa magonjwa yale yanayotokana na watu kugusana.
Kwa kuwa baadhi ya tafiti hizo zimefanywa na watafiti wa hapa nchini, bila shaka Serikali ijayo, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, itashiriki kikamilifu kuunda sera za kupiga marufuku matumizi ya makoti, hasa yenye mikono mirefu.

Post a Comment

Previous Post Next Post