Moshi. Sasa ni dhahiri kuwa
mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yanayofanyika leo
yatamkutanisha kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa
tangu waziri huyo mkuu wa zamani ajiondoe CCM na kujiunga na Chadema.
Ingawa
ratiba ya JK haikuwekwa wazi, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga
alisema Rais atawasili wilayani Mwanga leo mchana.
“Tunatarajia
Rais atawasili wilayani kwetu mchana na tunatarajia ibada itaanza saa
7:00 mchana. Shughuli za kuaga mwili hapa Usangi zitaanza saa 3:00
asubuhi katika Usharika wa Kivindu,” alisema.
Habari
zaidi kutoka kwa mmoja wa wanafamilia zinasema kuwa Rais atawasili kwa
helikopta. Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya
Awamu ya Nne, anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro leo saa 2:00 asubuhi na kwenda moja kwa moja na msafara wa
magari hadi Usangi wilayani Mwanga kwa ajili ya mazishi hayo.
Vigogo
wengine waliothibitisha kuhudhuria mazishi hayo ni pamoja na waziri
mkuu mstaafu na baba wa Jimbo la Mwanga, Cleopa Msuya, Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro na Lowassa.
Kwa kawaida
shughuli za mazishi huwa hazichukui mwelekeo wa kisiasa na ni kawaida
mahasimu kukutana, kuongea na kusalimiana, lakini tukio la leo litakuwa
likifuatiliwa kutokana na matukio ya hivi karibuni ya wawili hao ambao
hawakukutana “barabarani”.
Vigogo hao wanakutana, ikiwa
ni siku nne tu baada ya Lowassa kumtaja hadharani Kikwete kuwa
ameharibu uchumi wa nchi kwa kushindwa kusimamia mfumuko wa bei za
bidhaa mbalimbali ambazo ni muhimu kwa wananchi.
Akimpokea
mgombea urais wa CCM, John Mafuguli baada ya kuchukua fomu za urais
kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Kikwete, bila kumtaja
Lowassa, alisema: “Mtoto wako akikukosoa na kuungana na maadui,
unamshughulikia pamoja na maadui hao ili kumwonyesha kuwa wewe ni baba
yake.”
Kutofautiana kwao kulianza mara baada ya Kamati Kuu ya CCM kumuengua Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Akiwa
mwenyekiti wa CCM, Julai 11 mjini Dodoma, Kikwete aliongoza kikao cha
Kamati Kuu kilichoengua jina la Lowassa, ambaye alikuwa akipewa nafasi
kubwa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutokana na kuwa na
uzoefu na kukubalika kwa wanachama kulinganisha na makada wengine 38.
Kuenguliwa
kwa jina lake kulisababisha rabsha kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya
CCM, ingawa baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuendelea na
mchakato.
Baadaye Lowassa alitangaza kuihama CCM na
kujiunga na Chadema ambayo ilimpa fursa nyingine ya kuendelea na ndoto
yake ya kutaka kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Tangu
wakati huo, wanasiasa hao wawili, ambao waliwahi kupachikwa jina la
Boys ll Men kutokana na kwenda pamoja kuchukua fomu za kuwania urais kwa
tiketi ya CCM mwaka 1995, hawajawahi kukutana hadharani.
Jina
la Lowassa lilikatwa pamoja na makada wengine 32 katika hatua za awali,
lakini, kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM
walizungumza hadharani kuwa katiba ilikiukwa, wakisema si majina yote
yaliyowasilishwa kwenye kikao hicho.
Tamko la wajumbe
hao lilifuatiwa na kitendo cha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo
wa kuwa na imani na Lowassa wakionyesha kupinga uamuzi wa Kamati Kuu,
wakati Rais Kikwete na wageni wengine wakiingia kikaoni, tukio ambalo
mwenyekiti huyo wa CCM alilielezea kuwa “haijawahi kutokea”.
Waziri
wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli, ambaye pia anatarajiwa kuhudhuria
mazishi hayo, ndiye aliyepitishwa kugombea urais baada ya kuwashinda
makada wengine wanne waliopitishwa na Kamati Kuu ambao ni Asha Rose
Migiro, Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe.
Katika
hatua nyingine, mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Kilimanjaro, Peter
David amesema kifo cha Kisumo ni pigo kwa CCM hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Ni mtu asiyeogopa jambo lolote na hapendi uonevu kwa mtu yeyote wala dhuluma,” alisema David.
Kada
huyo alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada iliyofanyika Usharika wa Moshi
Mjini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kulipofanyika
ibada maalumu la marafiki kuaga mwili wa Kisumo.
Askofu Martin Shao, ambaye alikuwa akiongoza Dayosisi ya Kaskazini, alisema Kisumo alikuwa ni mcha Mungu.
Post a Comment