Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku tisa kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, kuna dalili za wazi kuwa vyama vilivyosimamisha wagombea urais vinakabiliwa na kazi ngumu ya kuwafikia wananchi kutokana na muda mfupi uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa ratiba
ya NEC iliyotolewa Juni mwaka huu, wagombea wote wa nafasi za urais,
ubunge na udiwani watalazimika kutumia siku 64 kukamilisha kampeni zao
kuanzia Agosti 22 hadi Oktoba 24.
Kwa nchi
yenye eneo la kilomita 945,087 za mraba, barabara nyingi mbovu hasa
kwenye maeneo ya vijijini na umbali mrefu kutoka wilaya moja hadi
nyingine, jimbo na jimbo, muda huo, wa siku zisizopungua 60 zinazotakiwa
kisheria, utakuwa mwiba mchungu kwa wagombea wa urais ambao watataka
kuifikia sehemu kubwa ya nchi kunadi ilani na sera za vyama vyao na
kuwapigia debe wagombea wao wa ubunge na udiwani.
Ukilinganisha na muda wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010, muda huo ni pungufu kwa siku tano.
Ili
kuzifikia kata zote 3,957 za uchaguzi, majimbo 265 au wilaya zote 135,
ukiacha wilaya mpya zilizoongezwa na Rais Kikwete mwezi uliopita,
wagombea wote watatakiwa wavishinde vikwazo hivyo vya ubovu wa barabara,
rasilimali fedha na muda wa kupumzika kutokana na kuhitajika kusafiri
usiku na mchana kutumiza azma zao.
Kimahesabu, iwapo
watapanga kupita kila kata, watahitajika kuhutubia kata 62 ndani ya saa
12 zinazoruhusiwa na NEC kufanya kampeni kwa siku, hali ambayo itaweka
rehani afya zao na kuathiri ufanisi wa kampeni zao.
NEC
imebainisha katika tangazo lake la hivi karibuni kuwa Tanzania ina
jumla ya kata 3,957 ambazo zitashiriki uchaguzi mwaka huu.
Hata
kama wagombea hao wa urais na wagombea wenza watajipanga kufika makao
makuu pekee katika kila jimbo nchini, kwa aina yoyote ile ya usafiri,
watahitaji kutembelea wastani wa majimbo manne kila siku.
Hata
hivyo, ahueni kidogo inaweza kutokea iwapo wagombea hao wataamua kuuza
sera zao kwa kuigawa nchi katika wilaya na hivyo kutakiwa kuzunguka
wilaya mbili kila siku ili kukamilisha zaidi ya wilaya 133 zilizopo.
Katibu
mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan
Doyo aliliambia gazeti hili jana kuwa kuna ugumu katika kampeni za mwaka
huu, lakini wamejipanga kwa kutumia usafiri wa ardhini na angani
kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Kwa mwezi mmoja na
nusu tutatumia magari na muda uliobakia mgombea urais na mgombea mwenza
wataanza kutumia helikopta. Safari yetu ya kampeni itaanzia mkoani Tanga
Agosti 30 na bila shaka tutafanikiwa kwa asilimia kubwa,” alisema Doyo.
Wakati
ADC wakijipanga kutumia anga kukimbizana na muda, Chama cha Kijamii
(CCK) kilichomsimamisha Dk Godfrey Malisa na mgombea mweza Ali Said
Juma, kimesema kitatumia barabara “mpaka kieleweke”.
Mwenyekiti
wa CCK, Constatine Akitanda alisema pamoja na siku za kampeni kuwa
chache, watajitahidi kuhakikisha kila sehemu ya nchi wanafika kumnadi
mgombea wao wa urais.
“Sisi tutashambulia ardhini tu
hakuna sababu ya kwenda angani kwa sababu mambo yote ya wananchi yapo
chini. Tumeshagawana timu, tutapita nchi nzima hatutaacha jiwe ambalo
halijageuzwa,” alisema Akitanda.
Mkurugenzi wa Mafunzo
na Uchaguzi wa Chadema, Benson Kigaila alisema siku 64 zitawatosha
wagombea wa ubunge na udiwani lakini si kwa urais.
“Hata
useme unafanya kampeni katika majimbo 265 yaliyopo na kupanga kuzunguka
majimbo manne kwa siku, hutayamaliza,” alisema Kigaila huku akijigamba
kuwa “watamchinja ng’ombe kama alivyolala”.
“Lakini kwa
sababu muda umeshapangwa, sisi tutakabiliana nao hivyo hivyo hata kama
ni siku 10. Tutatumia magari na chopa kama ilivyo jadi yetu,” alisema.
Hata
wakati vyama vya siasa vikihofia muda kuwa mfupi, mwenyekiti wa NEC,
Jaji Damian Lubuva alitetea kuwa muda huo ni halali na zipo ndani ya
wigo wa sheria unaotaka kampeni zifanyike kwa siku 60.
“Hakuna
cha upungufu wa siku hapo, tulishafanya hesabu za kina ndiyo maana
ilitolewa ratiba hiyo. Jaribu kuangalia wanamalizia Agosti, wana mwezi
mzima wa Septemba na Oktoba, ni nyingi sana hizo na zipo kisheria japo
wengine huwa wanalalamika kuwa wanakuwa ‘exhausted’ (wanapata uchovu),”
alisema Lubuva.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Respicius Damian alisema kutokana na
mwamko wa kisiasa na ushindani uliopo baina ya vyama, siku hizo ni
chache na hivyo zitaathiri vyama na wapiga kura.
Alisema
tatizo la ubovu wa miundombinu mara nyingi huchangia mikutano ya
kampeni ichelewe kuanza katika maeneo mengi licha ya muda wa kumaliza
mikutano hiyo kubaki pale pale.
“Uchaguzi huu
unahusisha vigogo wakuu wawili (mgombea wa urais CCM, Dk John Magufuli)
na mgombea wa Ukawa kupitia Chadema (Edward Lowassa) ambao wanafahamika,
lakini wangehitaji muda zaidi kuzungumza na wananchi.
“Ratiba
hiyo inabana kwa sababu kutakuwa na maswali mengi sana kwa wagombea na
iwapo wanaojinadi hawatapata muda wa kutosha kujieleza, kuna kila dalili
za kuibuka kiwango kikubwa cha propaganda,” alisema Damian.
Pamoja
na wanasiasa na wataalamu kueleza kuwepo kwa mikimiki ya kampeni
kutokana na uchache wa siku, mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kiraia ya
Concern For Development Initiative Africa (Fordia), Buberwa Kaiza
alisema siku 64 ni nyingi iwapo vyama vitajipanga vizuri.
Buberwa,
ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi, alisema kama vyama
vingejitanua mikoani na kutumia njia nyingine za mawasiliano kama vyombo
vya habari, hakuna haja ya wagombea wa urais kufika kila eneo la nchi.
“Jambo
la msingi ni kufikisha ujumbe kwa wananchi, waelewe sera na kujibiwa
maswali yao yote na siyo wingi wa siku. Mwezi mmoja unatosha kabisa,
tatizo vyama havina mipango hata kama wakipatiwa miezi minne
haitavitosha,” alisema Kaiza.
Post a Comment