Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema Chadema inawasumbua kutokana na madai yao ya mara kwa mara, lakini chama hicho kikuu cha upinzani hakijakoma; kimeitaka Tume kujibu mambo matano kuhusu Uchaguzi Mkuu.
Chadema,
ambayo inashiriki Uchaguzi Mkuu ikiwa ndani ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), pia kimesisitiza kuwa wanachama na wafuasi wake
wataendelea kukaa mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura kama
walivyoagizwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
Chadema
imekuwa ikitoa matamko mbalimbali yanayoonyesha wasiwasi kuwa uchaguzi
hautakuwa huru na wa haki na katikati ya wiki, walitaka NEC iwakubalie
waende na wataalamu wao wa Tehama pamoja na waangalizi wa kimataifa ili
kukagua mfumo ambao Tume itautumia kupokea matokeo kutoka vituoni.
Ombi
hilo lilimfanya mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kusema Chadema
inawasumbua, akieleza kuwa kila wanapofanya jambo, chama hicho hufanya
kitu kingine.
Jana, Chadema iliibuka na tamko jingine ikiitaka Tume kujibu mambo matano kuhusu uchaguzi ambao utafanyika Oktoba 25.
“Tunataka kila jambo liwekwe wazi,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akiongea na waandishi wa habari jana.
Mnyika
alisema Chadema inaitaka Tume hiyo kutaja tarehe watakayovipatia vyama
vya siasa nakala pepe ya Daftari la Kudumu la Wapigakura, na tarehe
ambayo vyama vitakwenda ofisi za NEC na wataalamu wao wa Tehama kukagua
programu itakayotumiwa kuhesabu kura.
Pia
alisema wanataka maelezo ya sababu za tume hiyo kupinga wananchi kukaa
mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura, kutaka maelezo kama vyombo vya
habari na wadau wengine wataruhusiwa kujumlisha matokeo ya uchaguzi huo
na sababu za kubagua wanahabari kufika katika vituo vya kupigia kura
badala yake kutaka wale wenye vitambulisho vya serikali pekee.
Wakati
chama hicho kikiibuka na masuala hayo, Jaji Lubuva alisema watakutana
na vyama vyote vya siasa kati ya Oktoba 8 na 10 kufafanua masuala
mbalimbali, huku akisisitiza kuwa tatizo la Chadema ni kutaka kuingia
jikoni na kujua kila jambo linalofanywa na tume.
Katika ufafanuzi wake wa jana, Mnyika alisema: “Kwanza,
tunataka tupewe nakala za daftari la wapigakura za awali na za sasa ili
tuhakiki kama hakuna majina feki. Tunataka daftari hili liwe wazi pia
ili wananchi wahakiki majina yao maana yale yanayobandikwa katika vituo
vya kupigia kura ambayo NEC wamesema yatabandikwa siku ya nane kabla ya
uchaguzi ni orodha tu.”
Alisema
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, vyama vya siasa vilipewa nakala
hizo mapema na kuzihakiki, akifafanua kuwa faida ya daftari hilo
kutolewa mapema ni kuwapa fursa wananchi ambao majina yao hayataonekana
kufuatilia mapema ili kutopoteza haki yao ya kupigakura.
“Pili,
tunataka NEC iseme siku ambayo wataalam wetu watakwenda kukagua
programu itakayotumiwa na tume kuhesabu kura. Tunataka mifumo yote
miwili waliyoisema tuihakiki kama ipo sawa kuepusha uchakachuaji wa
matokeo na tunafanya hivi kwa sababu mifumo iliyotumika 2010 ilikuwa
mibovu,” alisema Mnyika.
Mnyika
alisema jambo la tatu ni kupingana na kauli za kuwazuia wananchi kukaa
mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura akisema suala hilo ni lazima
liruhusiwe ili kuwapa fursa wananchi kulinda kura zao zisiibiwe.
Alisema
jambo jingine ni NEC kueleza kama vyombo vya habari, asasi za kiraia na
waangalizi wa uchaguzi wataruhusiwa kujumlisha matokeo.
“Hili jambo ni muhimu maana matokeo ya urais hayahojiwi mahakamani, hivyo ni lazima tudhibiti ujanja ujanja mapema,” alisema.
Akijibu madai yaliyotolewa na Chadema, Jaji Lubuva alisema:
“Kama wana malalamiko wayalete ofisini kwetu. Siwezi kujibu malalamiko
yanayowasilishwa katika mikutano ya waandishi wa habari. Kifupi ni
kwamba tutakutana na vyama vyote vya siasa kuvieleza tulipofikia. Hawa
Chadema wanatusumbua sana hawa.”
Kauli ya Kova
Wakati
Chadema ikisisitiza msimamo wao, kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jeshi hilo limejipanga ipasavyo
kuelekea siku ya kupiga kura, akisema watakaobainika kukiuka sheria na
taratibu za uchaguzi watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
“Tunaomba
kila mmoja kufuata utaratibu utakaowekwa. Atakayeuvuruga hatutasita
kumchukulia hatua. Tunataka uchaguzi ufanyike kwa amani na kila mmoja
mwenye haki ya kupiga kura, apige kwa amani,” alisema.
Kuhusu
taarifa za kiitelijensia za kuwepo na watu kufanya vurugu, Kamishna
Kova alisema hawezi kurudia maneno yaliyosemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadiki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa, aliyesema watakaovunja sheria watakumbana na mkono
wa sheria.
Sadiki alonga
Sadiki
alisema kuwa kuna vikundi vimejipanga kufanya vurugu kwenye uchaguzi na
akavitaka kuacha mara moja kwa kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga
kukabiliana navyo.
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa hakuwa tayari kuvitaja vikundi hivyo wala kufafanua vinaratibiwa na nani.
Akifungua
semina ya mafunzo ya siku mbili ya wasimamizi 60 wa Uchaguzi Mkuu
kutoka wilaya tatu za Kinondoni, Temeke na Ilala, Sadiki alisema vikundi
hivyo vinatoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.“Tumejipanga kisawasawa kukabiliana na aina yoyote ya vurugu siku hiyo,” alisema Sadiki.
“Lengo
lao kubwa ni kuwatisha watu watakaopiga kura hususani kinamama na
wazee. Nawaomba waache mara moja kwani wakibainika watapambana na mkono
wa dola.
“Tunayatambua maeneo ambayo watapelekwa na tutahakikisha ulinzi unaimarishwa kwani tumejipanga ipasavyo.”
Alisema
mbali na hivyo, kundi jingine limejipanga kukaa mita 100 kutoka katika
kituo cha kupigia kura na kwamba wamepata taarifa kuwa watajipakaa rangi
zenye mfano wa damu na kuwatisha wananchi kwa kuwaambia kuna machafuko
kutokana na mwonekano wao.
“Nawaomba
wakishapiga kura, wananchi waondoke mapema vituoni. Ingawa sheria
inaruhusu kukaa mita 100, tunataka kupambana na mbinu hizi
zilizopangwa,” alisema Sadik.
Pia
aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia uwazi na kuhakikisha vituo
vinafunguliwa mapema ili kuondoa wasiwasi kwa wapigakura.

إرسال تعليق