Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.
Na Haruni Sanchawa
KUFA kufaana? Tukio la ajali lililosababisha kifo cha aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila
(pichani) limeendelea kuibua mazito baada ya familia ya marehemu huyo
kubaini kuwa, kadi ya benki ya Mtikila haikuwepo kwenye mkoba wake.
Baadhi ya vitu ambavyo familia hiyo ilichukulia kipaumbele kufuatilia
ilikuwa ni simu na kadi ya benki ambayo ilikuwa ni muhimu kuliko vyote
ndani ya mkoba wake aliosafiria siku chache kabla ya ajali.
Akizungumza na Uwazi juzi, Naibu Katibu Mkuu wa DP, Abdul Juma
alisema yeye kama kiongozi wa chama na familia ya marehemu Mtikila
walifuatilia vitu vilivyokuwemo kwenye mkoba wa kiongozi huyo ambapo
wanaamini ndani yake mlikuwa na kadi ya benki.
“Ndugu Mwandishi kazi hiyo ya kufuatilia ilifanyika siku ya Jumatatu
(Oktoba 12) lakini ndani ya mkoba wake kadi ya benki haikuwemo kitu
ambacho kilitushtua hadi hivi sasa,” alisema Juma.
Kiongozi huyo alisema kuwa, baada ya ajali hiyo, ule mkoba wake
ulipelekwa nyumbani kwa Mtikila na aliyeupeleka ni Mchungaji Mgaya
ambaye kwenye ajali hiyo alinusurika.
Uwazi lilibaini kuwa, kadi hiyo ilikuwa ni ya Benki ya NMB Tawi la
Bank House yenye namba 15110006438 ambapo familia hiyo inaamini kuwa
kulikuwa na kiasi kikubwa cha pesa ingawa iligoma kutaja idadi.
Juma aliongeza kuwa, katika mazingira ya kawaida kuna mtu anatuhumiwa
lakini si vyema kumtaja kwa jina kwa sababu za kiuchunguzi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Jafari Mohamed
alipoulizwa kuhusiana na kadi hiyo alisema hajapata malalamiko kutoka
kwa familia ya marehemu na kama kuna tatizo lolote ameitaka familia hiyo
kufika ofisini kwake kwa maelezo zaidi.
Mchungaji Mtikila alifariki dunia Oktoba 4, mwaka huu kwa ajali ya
gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Bagamoyo, Pwani na kuzikwa
kijijini kwake, Maro, Ludewa mkoani Njombe

إرسال تعليق