BAADHI
ya watu walimtafsiri Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP) na Mchungaji
wa Kanisa la Full Salvation, Christopher Mtikila kama hazimtoshi f’lani
hivi.
Lakini siku zote fikra ni utumwa wa mtu mwenyewe. Sikuwahi
kuwashangaa waliomkebehi kwa jambo lolote Mtikila wakati wao hawawezi na
hawataweza kuonesha ujasiri wa kiwango cha robo ya mwanasiasa huyo.
Mtikila
ninayemzungumzia ni mtu pekee aliyewahi kuishtaki serikali ya nchi hii
na kuishinda. Narejea kesi ya mgombea huru aliyoifungua mahakama kuu na
baadaye kuipeleka mahakama ya Afrika.
Wakati anashughulikia kesi hii ya mgombea huru mwaka 2013, niliwahi
kumuuliza ugombea binafsi ulihusu nini hasa? Nilijua yeye ana chama
chake.
Majibu aliyonipa: “Mimi sina tatizo, lakini siwezi kuwa kiongozi
ninayetetea masilahi yangu, mimi nataka kila Mtanganyika awe na haki ya
kuchagua na kuchaguliwa sawa na katiba inavyotamka.”
Huyu ndiyo shujaa Mtikila aliyekufa akipambana kutetea haki za
wananchi wanyonge kwa kufungua marundo ya kesi za kikatiba na kijinai
dhidi ya kile alichoamini ‘haki haiombwi.’
Suala la kutafuta haki halikuwa jambo lililohitaji malipo kwa
Mtikila; mwanasiasa huyu alikuwa tayari kupanda pikipiki, Bajaj au hata
kutembea kwa miguu kwenda mahakamani kudai haki za wengi.
Alipofungua kesi ya kudai uhuru wa kufanya mikutano bila kuomba
kibari cha polisi kama utaratibu ulivyotaka, mara kadhaa alikwenda
mahakamani kwa kupanda magari ya usafiri wa umma.
Wapo waliomtafsiri vibaya, wakambatiza majina kibao ya kejeli,
mpendakesi, mpuuzi, mwendawazi, mganga njaa na mambo mengimengi ya
kumfedhehesha.
Kupenda kwake kesi kumelisaidia taifa katika mambo mengi mojawapo ni
kupata uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara bila kuomba kibari polisi,
jambo ambalo vyama vyote vya siasa vinanufaika nalo hadi ‘mganga njaa’
anaingia kaburini. MASKINI!!!
Sote ni wasafiri wa kurudi udongoni; apumzike kwa amani Mtikila
ambaye kila nilipokutana naye nilijifunza jambo muhimu kiasi cha kuamini
kuwa, upuuzi wake ulikuwa na faida kwa taifa kuliko werevu usio na
msaada.
Mtikila hakuwa muoga, ilihitaji ujasiri na fikra pana kuzungumza
naye, kumwamini na kumuelewa hasa pale alipotaja bila hofu dhambi za
viongozi mbalimbali wa ngazi za juu serikalini, kimataifa na wa dini
zote na kuwa tayari kukabiliana nao kwa ajili ya kulinda masilahi ya
nchi.
Kabla ya kufanyika kwa Oparesheni Kimbunga iliyolenga kuwaondoa
wahamiaji haramu, Mtikila alisambaza waraka akimtuhumu Rais Paul Kagame
na Wanyarwanda kuwa wamevamia sehemu ya ardhi ya nchi yetu na hivyo
kuitaka serikali kuchukua hatua.
Mtikila aliniambia waraka huo alimpelekea pia Rais Jakaya Kikwete.
Sijui aliupokea au la lakini kilichotokea Wanyarwanda waliokuwa maeneo
mbalimbali ikiwemo Ngara mkoani Kagera walirejeshwa makwao; huu ndiyo
ushujaa wa Mtikila.
Mtikila amekuwa shujaa aliyepitiliza; waoga walijiuliza ujasiri wa
kufanya ukosoaji mkubwa namna ile aliupata wapi; je hakuogopa kuuawa?
Majibu yake kila mara yalikuwa: “Watu waovu katika nchi yetu
hawapaswi kupewa nafasi, lazima washughulikiwe na unaposhughulika nao
kufa ni sehemu ya mapambano.”
Septemba 30, mwaka huu majira ya mchana Mtikila alipita ofisini
kwangu kuniaga (maana sikujua kama atafariki dunia Oktoba 3) aliniambia:
“Tumieni magazeti yenu kuleta ukombozi wa nchi, mna magazeti mengi,
andikeni kila gazeti kuhusu siasa, magazeti yenu yanaweza kuleta mageuzi
makubwa kwenye nchi hii.”
Nadhani huu ndiyo wosia aliotuachia kama chombo cha habari kwamba
tufanye kazi ya kuleta mageuzi ya kifikra, tuwe watu wa kutetea haki za
wanyonge kama alivyofanya yeye. Pumzika Mtikila; tutaendelea kujenga
ulipoishia!
إرسال تعليق