Dk. Emmanuel Makaidi enzi za uhai wake.
MWENYEKITI Mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa chama cha NLD, Emmanuel
Makaidi amefariki dunia leo mchana kwa shinikizo la damu akiwa Hospitali
ya Nyangao mkoani Lindi.
Wasifu wake
Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati
ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati
(Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye alijiunga na
Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha
kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958.
Baada ya hapo alielekea Afrika Kusini na kujiunga na Chuo Kikuu cha
Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya
mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa
masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na kusoma
masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka
1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini
Washington, Marekani.
Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi
serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika
kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na
kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa katika Chuo
Kikuu cha Howard.
Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake
pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi,
akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa
inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Baada ya hapo aliendelea na kazi serikalini ila kuanzia mwaka 1992
hadi mauti yanamfika, Dk Makaidi hajajishughulisha tena na kazi za
serikalini wala mashirika binafsi. Alikuwa amejiajiri akiwa na kampuni
kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini pia alikuwa
akitoa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya nchi
huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.
Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika zaidi ya vitabu 10.
Marehemu ameacha mke aitwaye Modesta Ponela na walibahatika kupata watoto wanane.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi . AMEN!

إرسال تعليق