TAARIFA ILIYOTOLEWA NA UMOJA WA VIJANA WA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 31 OKTOBA 2015 MAKAO MAKUU YA UVCCM DAR ES SALAAM
Ndugu Waandishi wa Habari,
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
unachukua nafasi hii kukipongeza kwa dhati Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
aliyekuwa mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais
mteule Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea mwenza wake Mhe. Samia
Suluhu Hassan kwa kupata ushindi wa kidemokrasia wa kishindo kwa kupata
asilimia 58.46%.
Ushindi huo ni alama na kielelezo cha
kuendelea kukubalika kwa CCM mbele ya Watanzania walio wengi kutokana na
Sera zake, Mipango yake na mikakati ya kuwatumikia wananchi, kulinda
amani, utulivu na kuendeleza Umoja wa Kitaifa nchini.
Ndugu waandishi wa habari,
Kwa upande mwingine tumelazimika kuwaita
hapa leo kuelezea masuala muhimu kadhaa yaliyojitokeza katika Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015.
Kama ilivyotolewa taarifa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, kwamba Uchaguzi
wa Zanzibar kwa sehemu kubwa ulikumbwa na kasoro nyingi za kimsingi
ambazo zimesababisha Tume kufuta matokeo kwa nafasi za Urais,
Wawakilishi na Madiwani.
Ndugu waandishi wa habari,
UVCCM tumefanya tathmini ya haraka na
kina ili kujua kiini cha tatizo hilo ikiwemo kukusanya taarifa toka
vyanzo mbalimbali ambapo tumebaini na kugundua madhaifu kadhaa
yaliyojitokeza katika hatua za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa
upande wa Zanzibar.
Tumepata wasiwasi wa suala zima la namna
zabuni ya karatasi za kupigia kura ilivyotangazwa na kumpata mzabuni
ambae alipewa kazi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Ni ukweli usiopingika kwamba ZEC
ilizidiwa nguvu na wanasiasa wa Chama cha Upinzani cha CUF ambao kwa
kiasi fulani wameshinikiza Tume ya Uchaguzi kwa namna moja au nyingine
kuikubali Kampuni ya ya Afrika Kusini ambayo sifa zake zinafahamika kuwa
ina matatizo.
UVCCM tuna mashaka na kampuni hiyo
iliyopewa kazi ya kuchapisha vifaa vya Uchaguzi ambayo kumbukumbu
zinaonyesha iliwahi kuomba kazi ya kutayarisha vifaa kama hivyo katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kupewa, lakini SMZ baada ya kugundua
kampuni hiyo ina matatizo, ilivunja mkataba na karatasi za kura
zilichapishwa hapa hapa nchini.
Kampuni hii inalalamikiwa kuwa chanzo
cha kuvurugika kwa chaguzi mbalimbali katika nchi za Afrika ikiwemo
Cameroon, Benin, Ivory Coast na baadhi ya nchi za Latini Amerika.
UVCCM tumeshangazwa sana kuona ZEC wakiikubali Kampuni ambayo tayari
SMZ mwaka 2005 waliikataa na kuvunja nayo mkataba.
Kampuni hii inasemekana kwamba imekuwa
inashirikiana na vyama vya upinzani hasa katika nchi za Afrika chini ya
mkakati wa kuvisaidia kushinda Uchaguzi.
Pia tumepata mashaka na watendaji wa
Tume ya Uchaguzi Zanzibar ama walizembea au walikuwa sehemu ya njama za
kutaka kuvuruga uchaguzi. Kwa nini tunasema hivyo? Ni kwa sababu
watendaji wa Tume ya Uchaguzi wanaifahamu vyema Kampuni hii, matatizo
yake, lakini wameshindwa kuishauri Serikali na matokeo yake kuiingiza
nchi katika hasara na mkanganyiko wa kisiasa.
Tunawataka watendaji wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar kujipima kama wanatosha kuendelea kuwa na sifa ya kuwa
Watendaji wa Tume hii sambamba na Makamishna wao ambao nao hawakujituma
zaidi kujiridhisha na utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa kuzingatia
taarifa za nyuma za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa pale ilipovunja
Mkataba.
Kwa mwenendo huo na mtazamo halisia ni
wazi kuwa Chama cha CUF kimehusika na njama hizi za wizi wa kura na ndio
maana Katibu Mkuu wake Seif Shariff Hamad akaamua kukiuka taratibu na
kajitangazia ushindi kinyume na Katiba na Sheria za nchi wakati zoezi la
kuhesabu kura likiendelea katika majimbo ya Pemba na Unguja. Ni kituko
na mshangao kuona vyombo vya dola vikimtazama macho mgombea huyo
aliyefanya kosa la jinai bila ya kumchukulia hatua za kisheria na
kumfikisha kwenye mikono ya sheria.
Umoja wa Vijana wa CCM tunaitaka
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kuunda Tume huru itakayochunguza kwa kina
na undani wa kadhia hii ikiwemo suala zima la namna ilivyoendeshwa
zabuni hadi kufikia kupatikana mzabuni na taarifa yake itolewe kwa umma.
Ndugu waandishi wa habari,
Tumekuwa tukisema mara kadhaa Chama cha
CUF ni chama ambacho kimezoea kuwahamasisha wafuasi wao kufanya vurugu,
ghilba, ubaguzi na masuala mengine ambayo hayaendani na kanuni za
kidemokasia.
Katika kuyathibitisha haya, wakati wa
kazi ya kupigakura na kuhesabu kura huko Kisiwani Pemba, wafuasi wa CUF
wakiwa na jazba wamevamia vituo vya kupigia kura kinyume cha sheria na
kuanza kuwashambulia kwa mapanga Mawakala wa Chama cha Mapinduzi na
kuwatoa nje, huku wengi wao wakijeruhiwa vibaya.
Wafuasi hao wa CUF wakiwa katika
makundi, wameyafanya hayo katika Vituo vya Majimbo ya Tumbe, Micheweni
na Konde katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo Mawakala wa CCM
wamewapiga na kuwajeruhi na kusababisha kusimamishwa kwa kazi za
kuhesabu kura.
Hadi sasa Mawakala wetu hali zao sio
nzuri bado wapo hospitalini wakiendelea kupatiwa matibabu. Tumekuwa
tukijiuliza inakuwaje Pemba CUF hawataki vyama vyengine kushiriki
Uchaguzi kwa kuwafanyia vitendo vya kuwapiga, kuwabagua, kuwabughudhi
wakati wao wanashiriki katika kila uchaguzi ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania?
Ndugu waandishi wa habari,
Haikuishia katika Majimbo hayo tu, bali
uvunjaji wa sheria uliendelea katika sehemu mbalimbali za huko Pemba
ambapo wafuasi wa CUF waliokuwa wamekaa pembezoni mwa barabara karibu na
Vituo vya Makangale, Kisiwani kwa binti Abeid, Chonga, Mtambwe, Wete,
Kojani, Mchangamdogo wafuasi hao wa CUF waliwazuia wana CCM wasiende
kupigakura.
Mbali na kufanya hivyo, pia katika
huduma za usafiri wafanyakazi wa gari za abiria za kutoka Wete kwenda
Gando, Konde-Wete, Chake – Wete kupitia njia kongwe waliwashusha wana
CCM na huku katika vituo vyengine vya kupanda abiria wakiwakataa wana
CCM wasipande magari yao
Hivi wanataka kutuambia kuwa CCM na
vyama vyengine nje ya CUF havina haki ya kushiriki katika Siasa Kisiwani
Pemba? Ubaguzi huu haukubaliki na tunawaomba wapenda demokrasia wote na
Jumuiya za Kimataifa kuchukia vitendo vya kibaguzi na kihuni
vinavyofanywa na wafuasi wa CUF kule Pemba.
Ndugu waandishi wa habari
Tangu siku ya Jumatatu wafuasi wa CUF
kule Pemba wanachanganya maji na dawa ya kusafishia chooni au kwenye
masinki ya kuoshea vyombo wanawamwagia wafuasi wa CCM ama katika makazi
yao au usiku wakiwa wamelala wanawamwagia maji hayo ambayo yanawaletea
madhara ya kuwashwa mwilini.
Ni dhahiri kuwa Chama cha CUF hakipati
kura nyingi kule Pemba kwa ridhaa ya wapigakura, bali ni kwa
kuwashurutisha wapigakura , kutoa vitisho na hata katika baadhi ya
Majimbo wanawake wametishiwa na waume zao wasipopiga kura CUF watapewa
talaka.
Hali kama hiyo pia imejitokeza katika
Shehia za Kijini na Potoa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo wanaume
waliwashurutisha wake zao kwamba watakapofika kituo cha kupigia kura
wadai hawajui kusoma na kuandika au wana matatizo ya kutokuona vizuri
ili waume zao wapige kura kwa Chama cha CUF. licha ya sheria kuzuia
mikusanyiko ya watu karibu na vituo vya kupigia kura huko Pemba wafuasi
wa CUF walikusanyika karibu na vituo vya kupigia kura Katika majimbo ya
Ole, kojani, Chonga, Mkanyageni, Mtambwe, Wete, Jadida, na Konde,. Vituo
vya shengejuu pujini, kiuyu, Minungw’ini kulikuwa na wafuasi wa CUF
waliokusanyika na hata walipotakiwa kuondoka na polisi hawakutii.
Ndugu waandishi wa habari,
Yote hayo yametendeka mbele ya macho ya
watendaji wa Tume ya Uchaguzi na licha ya mawakala wetu kulalamikia
ukiukwaji huo wa demokrasia hakuna aliyewasikiliza. Ni wazi kuwa
kuliandaliwa mazingira ya wizi wa kura na ukiukwaji wa taratibu na
sheria uliopewa baraka na baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar.
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi
tunalaani vikali vitendo vya wafausi wa Chama cha CUF na tunaziomba pia
Jumuiya za kimataifa kuungana nasi katika kulaani vitendo hivyo ambavyo
havikubaliki hata kidogo.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama
kuwasaka wale wote wanaohusika na uharamia huu na kuwafikisha katika
vyombo vya kisheria.
Sote tunafahamu kuwa misingi ya uchaguzi
huru ni pamoja na masuala mazima ya kutotishwa wapigakura,
kutoshurutishwa kupiga kura kwa Chama fulani kwa maana mpigakura awe
huru kuchagua Chama anachokitaka , kuwepo kwa mawakala na watazamaji
wengine wa Uchaguzi mambo ambayo kwa sehemu kubwa hayazingatiwi katika
Majimbo mengi kule Pemba.
Wakati tukijiandaa kurejea Uchaguzi wa
Zanzibar UVCCM. Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwa makini na watendaji wake
hasa wasimamizi wa vituo kule Pemba ambao kwa namna moja au nyingine
wanashirikiana na Chama cha CUF kuvihujumu Vyama vingine hasa Chama cha
Mapinduzi.
Ndugu waandishi wa habari,
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na pengine ilijulikana mapema na waangalizi wa Uchaguzi, Makundi ya Waangalizi wa Uchaguzi hasa wale wa Kimataifa walikipa kisogo Kisiwa cha Pemba. Tujiulizeni kwa nini waangalizi wengi walisalia katika Kisiwa cha Unguja na kukiacha Kisiwa cha Pemba?
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na pengine ilijulikana mapema na waangalizi wa Uchaguzi, Makundi ya Waangalizi wa Uchaguzi hasa wale wa Kimataifa walikipa kisogo Kisiwa cha Pemba. Tujiulizeni kwa nini waangalizi wengi walisalia katika Kisiwa cha Unguja na kukiacha Kisiwa cha Pemba?
Hata hivyo tunazo taarifa za uhakika
kuwa baadhi ya waandishi wa habari nao waliondolewa kwa hila na vitisho
huko Pemba kwa madai kuwa kungeweza kutokea machafuko ambayo
yangehatarisha aidha maisha au usalama wao .
Mpango huo wa vitisho tumepata ushahidi
umeratibiwa na kusimamiwa ipasavyo kwa karibu na waandishi wawili wa
habari wa kike ambao ni wafuasi na mashabiki wa CUF waliokuwa wakipokea
maelekezo kutoka kwa Kiongozi mmoja wa Upinzani huko Zanzibar.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
Post a Comment