
Dar na Lindi NI msiba! Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk. Emmanuel Makaidi (74), amefariki dunia jana saa 7 mchana katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi, saa chache kabla ya kuzikwa kwa Dk. Abdallah Kigoda nyumbani kwao, Handeni mkoani Tanga.
Habari kutoka Lindi zinasema Dk. Makaidi alifariki dunia kutokana na matatizo ya shinikizo la damu na zilithibitishwa na mkewe, Modesta Makaidi. Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyangao, Betram Makota alithibitisha kifo hicho na kusema Dk. Makaidi alifikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui na kabla ya kupatiwa matibabu, alifikwa na mauti. Dk. Makaidi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD) kabla ya kufikwa na umauti alikuwa anagombea ubunge Jimbo la Masasi Mjini mkoani Mtwara kwa mwamvuli wa Ukawa japokuwa wakati wa kampeni mjini humo alipata wakati mgumu baada ya kupingwa hadharani na wapiga kura mbele ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa. Dk. Kigoda, mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Handeni Mjini na ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, yeye alifariki dunia Oktoba 12, mwaka huu katika Hospitali ya Apollo, India alikolazwa kutokana na tatizo la saratani. Tangu Julai, mwaka huu, watu 16 waliokuwa kwenye harakati za siasa kuelekea uchaguzi mkuu wamefariki dunia ambapo miongoni mwao, 13 walikuwa wanawania nafasi za uongozi, hususan udiwani, ubunge na urais. Kumbukumbu zinaonesha kwamba, Conrad
Mtenga ‘Chillangamsafa’ (53), Mkaguzi wa Kanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ndiye aliyeanza kupatwa na mauti Julai 16, 2015 wakati akiwa njiani kwenda Njombe kutangaza nia ya kuwania ubunge. Ofisa huyo alifariki dunia katika ajali iliyotokea eneo la Tanangozi, Iringa baada ya gari lake kugongana uso kwa uso na lori. Aidha, Julai 27, 2015 kada wa Chadema aliyekuwa anataka kuwania ubunge Mjini Unguja, Bikwao Hamad, alianguka ghafla na kufariki dunia wakati akitoka nje baada ya kujieleza kwa wapigakura katika uchaguzi wa ndani.
Uchaguzi huo umetajwa kuandamwa na vifo vya wanasiasa ama wafuasi wao, kwani ni siku 12 tu zimepita tangu Mchungaji Christopher Mtikila, Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), ambaye pia alikuwa mgombea urais kabla ya kuenguliwa na Tume ya Uchaguzi (Nec), alipofariki dunia kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Msolwa wilayani Bagamoyo. Kifo cha Mchungaji Mtikila kimezua maswali mengi yasiyo na majibu, huku wengine wakisema aliuawa kwa sababu za kisiasa. Septemba 12, mwaka huu, mgombea ubunge wa Jimbo la Lushoto kupitia Chadema, Mohammed Mtoi Kanyawana (39) alifariki dunia kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea katika eneo la Magamba wakati akirejea nyumbani kwao, Mkuzi baada ya shughuli za kampeni jimboni humo. Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, alifariki dunia Septemba 24, 2015 katika Hospitali ya Apollo nchini India alikokuwa amelazwa kwa matatizo ya saratani. Kumbukumbu zaidi zinaonesha kwamba, Oktoba 9, 2015, mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Estomih Malla, alifariki dunia katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi baada ya kulazwa kwa siku mbili kwa tatizo la shinikizo la damu. Agosti, mwaka huu, kada wa Chadema katika Jimbo la Sengerema, Dk. Shadrack Watugala, alifariki dunia baada ya kuanguka nyumbani kwake, Migombani,
Sengerema wakati akitokea kanisani. Alikuwa ametangaza nia kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema. Mnamo Agosti 30, 2015, Livingstone Nkya ‘Ferefere’, mgombea udiwani wa Kata ya Boma Ng’ombe wilayani Hai kupitia CCM, alifariki dunia katika Hospitali ya KCMC. Mara baada ya kuzindua kampeni, alijisikia vibaya na kwenda mwenyewe Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, baadaye akahamishiwa KCMC alikofia. Septemba 14, mwaka huu mgombea udiwani wa CCM katika Kata ya Uyole jijini Mbeya, Kambi Njela, ambaye alikuwa amepita bila kupingwa, alifariki ghafla wakati akiwa kwenye kampeni za kuomba kura. Aidha, Septemba 20, mwaka huu, Osward Rwakabwa, mgombea udiwani wa Kata ya Muleba kupitia CCM, alifariki dunia kwa ajali ya pikipiki (bodaboda). Taarifa zinaonesha kwamba, Oktoba 4, mwaka huu, Ofisa Uhamasishaji wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Erasmo Nyingi, alifariki dunia baada ya kupata ajali akiwa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyasa, Casbert Ngwata, baada ya gari lao kutekwa na majambazi. Kampeni za uchaguzi mwaka huu zimeshuhudia pia vifo vya wananchi wakiwa kwenye mikutano ya kisiasa ambapo Septemba 21, mkazi wa Ng’apa mjini Lindi, Fatu Jega, alifariki dunia ghafla akiwa kwenye mkutano wa kampeni za mgombea udiwani wa kata hiyo ya Ng’apa kupitia CCM, Mwanaidi Mbungo. Septemba 7, mwaka huu, watu wawili walifariki kwenye mkanyagano wakati wa mkutano wa mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli. Septemba 10, Mwita Mwange, mkazi wa Kijiji cha Ketonga wilayani Tarime, alifariki dunia kwa kukatwa mapanga baada ya kutokea vurugu baina ya wafuasi wa Chadema na CCM.
CHANZO: UWAZI MIZENGWE

إرسال تعليق