Highnes Kiwia Kupinga Matokeo Ya Mabula Mahakamani

 

ALIYEKUWA mgombea ubunge Jimbo la Ilemela, Highnes Kiwia, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ametangaza kwenda mahakamani kupinga matokeo yaliompa ushindi, Angelina Mabula (CCM).

Kiwia amesema kuwa matokeo yaliyompa ushindi Mabula yalikuwa ni ya kutengenezwa ili kumbeba mgombea huyo wa CCM kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiwia amesema atatumia haki ya kikatiba kupinga matokeo hayo mahakamani ili maoni ya wananchi kuheshimiwa na kupata haki zao za msingi.

Hata hivyo katika matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, John Wanga, alimtangaza Angelina Mabula mshindi kwa kura 81, 424 dhidi ya Kiwia aliyepata kura 61,679.

Kiwia pia amesema kuwa katika baadhi ya vituo majina ya wapiga kura yaliongezwa, mawakala wake kutishiwa na baadhi ya wafuasi wa CCM kitendo ambacho dhahili alidai uchaguzi haukuwa huru.

“Kuna vituo ambavyo majina yaliongezwa, zaidi ya majina 700 ya wapiga kura yalihamishwa na kupelekwa Ukerewe, baada ya kupata taarifa ya kuhamishwa majina tulitoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi lakini hatua hazikuchukuliwa.

“Matokeo haya yalikuwa yamepangwa kabla ya uchaguzi kufanyika, tunaenda mahakani kupinga matokeo haya, hatutaona maoni ya wananchi yanapotea,” amesema Kiwia.

Pia Kiwia alivitaja baadhi ya vituo ambavyo vilikuwa na kasoro kuwa ni pamoja na Kitangiri, Ilemela na Nyansaka na kwamba wamejipanga muda wowote kwenda mahakamani.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chadema, Kanda ya Ziwa Victoria, Tungaraza Njugu amesema matokeo ya uchaguzi huo sio sahihi na kwamba maoni ya wananchi walio wengi yameporwa na CCM.

Post a Comment

Previous Post Next Post