Chadema Wakanusha Habari Zinazoendea Mitandaoni Kuwa Wameenda ICJ na ICC Kuishitaki CCMZiko habari zimezushwa, kuenezwa na sasa zinakuzwa kuwa mgombea urais wa CHADEMA na chama kwa ujumla kimefungua shauri Mahakama za Kimataifa, kuhusu ubakwaji wa demokrasia na hujuma dhidi ya Watanzania uliofanyika kwenye Uchaguzi (uchafuzi?) Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Itoshe tu kusema kuwa hadi kwa hatua ya sasa habari hizo si za kweli. Ni uzushi.
Watawala, wanaotuhumiwa kupoka haki ya Watanzania ya kuchagua viongozi wanaowataka, wanajua dhambi waliyowafanyia wananchi ni sawa na ile hadithi ya Mzee Mvuvi kwenye Vitabu vya Alfu Lela Ulela, aliyefungulia jini kutoka kwenye chupa. Dhambi inawawinda. Mzimu wa walichokifanya unawaandama. Maana safari hii ukatili (kuvuruga uchaguzi) ulikuwa wazi wazi mno.
Wanajaribu kuchokonoa kujua ukimya wa Ndugu Edward Lowassa, kama mgombea chaguo la watu, CHADEMA, UKAWA na wapenda mabadiliko unaweza kuwa na kishindo gani! ICJ, ICC au wapi hasa!

Hivyo wanatunga tunga mambo na kusambaza wakitaka kupima hisia, fikra za wanamabadiliko waliotapakaa nchi nzima wakilia kilio cha kudhulumiwa haki katika uchaguzi, zinawaza nini! Maana hata wao wanashuhudia namna nchi ilivyokumbwa na msiba tangu walipotangaza matokeo yasiyooana na uhalisia wa hisia za wapiga kura na matakwa ya waliyo wengi katika demokrasia.
Tumelazimika kufafanua kuhusu uvumi huo kwa sababu umezidi kuenezwa kiasi cha vyombo vya habari kuanza kuulizia ukweli wake.
Baadhi ya watu waliotajwa kwa majina katika uvumi huo wako hapa nchini, wakiendelea na majukumu, hususan vikao vya Kamati Kuu ya dharura, ambayo imekuwa ikikutana jijini Dar es Salaam.
Chama kilipoandika barua kwenda Jumuiya ya Kimataifa, kuhusu hatari iliyokuwa inawekwa na watawala katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kupitia kauli za vitisho, matendo yao ya kujiandaa kuharibu uchaguzi, BVR, mfumo wa ujumlishaji matokeo n.k, tuliutaarifu umma wa Watanzania kupitia vyombo vya habari na njia zingine za upashanaji habari. Kwa sababu si siri.

Ukifanywa uamuzi mwingine wowote ule kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kupigania haki yao iliyoporwa katika uchaguzi mkuu, umma wa Watanzania ambao ndiyo wenye mamlaka katika nchi, utashirikishwa.

Makene

No comments:

Post a Comment