NYALANDU:HONGERA ASKARI KWA KUMNASA JANGILI SUGU



Jitihada za serikili kwenye mapambano dhidi ya ujangili zinaendelea kuzaa matunda baada ya Kikosi cha Kupambana na Ujangili kumkamata mtuhumiwa mkuu wa ujangili anayejulikana kama Shetani.

Kukamatwa kwa jangili huyo kumetokana na jitihada za usiku na mchana zilizofanywa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine hususan askari wa wanyamapori kwa kipindi cha mwaka mmoja kwenye maeneo mbalimbali ya uhifadhi nchini.

Akizungumza wakati akielekea jijini London, Uingereza kwa safari ya siku mbili ya kikazi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kazi iliyofanyika ni kubwa na inastahili pongezi.

Alisema majangili wamekuwa wakiisumbua serikali kwa kipindi kirefu lakini kutokana na jitihada za serikali na wadau wengine zikiwemo nchi wahisani wa maendeleo na jumuia za kimataifa hali inaendelea kuwa nzuri.

Alisema Shetani anakuwa wa pili kukamatwa baada ya Queen of Victory aliyekamatwa na serikali kipindi cha nyuma akiendelea na jitihada za kufanya uhalifu wa kuua na kuiba viungo vya wanyamapori wa Tanzania.

Waziri Nyalandu alisema serikali itaendelea na mapambano ya kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria vigogo wa ujangili na wanaowasaidia kufanikisha uhalifu huo hapa nchini.

Alisema akiwa jijini London atahudhuria mkutano wa Mawaziri wa Utalii kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika Mashariki, ambao watazungumza mambo mbalimbali yanayohusu namna za kuendeleza sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema pia mkutano huo utahudhuriwa na Mwanahabari maarufu wa Shirika la Habari la CNN, Richard Quest atakayefanya mahojiano maalumu kuhusu masuala ya Utalii na Maliasili.

Kuhusu hali ya siasa nchini, Nyalandu alisema uchaguzi umeisha na  kwamba viongozi walioshinda wanapaswa kufahamu kuwa si wao walioshinda bali ni watanzania kwa ujumla hivyo wawe wamoja kuijenga Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post