Pep-Guardiola-Bayern-Muni-014
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola (pichani) amesema anataka kupata changamoto mpya katika maisha yake ya soka na anataka kwenda kufundisha Uingereza baada ya kugoma kuongeza mkataba Bayern Munich na nafasi yake kuchukuliwa na Carlo Ancelotti.
Vilabu vya Manchester United, Mancheter City na Chelsea vyote vya Uingereza tayari vinaonekana kumuhitaji kocha huyo wa zamani wa Barcelona ambaye anaonekana kupata mafanikio kwa klabu zote ambazo amekuwa akizifundisha hali inayovifanya vilabu vingi kuhitaji kumpata kocha huyo raia wa Hispania.
Guardiola ameweka wazi mipango yake ya kufundisha klabu za Uingereza katika mkutano wake na waandishi wa habari na kusema kuwa anataka kupata changamoto mpya ya soka na anapendelea kwa sasa kufundisha klabu za Uingereza.
“Nahitaji changamoto mpya na ninataka kutumia nafasi hiyo kuwa meneja wa klabu za Uingereza, nataka kuzoea hali ya Uingereza na kuangalia mbele zaidi katika viwanja, nina miaka 44 kwa sasa nadhani ni muda sahihi lakini bado sijasaini kwa klabu yoyote, nitakapopata klabu mpya nitaweka wazi ili kila mtu aijue,” alisema Guardiola.
Aidha baadhi ya vyombo vya habari vimekua vikimuhusisha kocha hiyo na klabu ya Manchester City ambayo nayo inatajwa kumuhitaji kocha huyo pamoja na wapinzani wao Manchester United na Chelsea ambayo wiki kadhaa zilizopita walimtimua aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho na kumchukua Guus Hiddink kwa mkataba wa muda mfupi hadi utakapomalizika msimu wa 2015/2016.
Baada ya Manchester City kuhusishwa zaidi na Guardiola, Kocha wa Man City, Manuel Pellegrini ameulizwa na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Guardiola kutaka kufanya kazi Uingereza na kujibu “Sina uamuzi wowote kuhusu hilo au hata kuhusu mameneja wengine,” alisema na kuongeza “Ni swali ambalo nililijibu wiki mbili zilizopita wakati niliposema siyo sahihi kuhusu hilo [Guardiola kuchukua nafasi yake]”