IMG_1615
Pichani ni Mohammed Dewji alipokuwa mgeni rasmi wa tamasha la Simba Day, akisalimiana na mmoja wa wadau kwenye jukwaa kuu. Kulia ni Nyange Kaburu.  (Picha na Maktaba yetu).
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Mmoja wa mashabiki wa wakongwe wa klabu ya Simba, Stanbul Mponda amemuomba Bilionea namba moja nchini, Mohammed Dewji ‘MO’ kuendeleza mipango yake ya kuinunua Simba ili aweze kufanya uwekezaji kama alivyokuwa amepanga awali.
Mponda ameyasema hayo ikiwa ni siku chache zimepita za tarehe ya mwisho ambayo aliiota MO kwa uongozi wa Simba kutoa majibu kama wanamuuzia hisa za klabu hiyo na kama watakuwa hawajatoa majibu atafutilia mbali mpango wake wa kuinunua Simba.
Akizungumza na kipindi cha michezo cha E Sports kinachorushwa na redio ya E Fm, Mponda alisema wanafahamu kuwa MO amekuwa mtu ambaye ana mapenzi ya dhati na Simba na hivyo kucheleweshwa kutolewa kwa majibu na uongozi wa Simba isiwe sababu ya yeye kuacha kuinunua klabu hiyo kongwe nchini.
“Dewji ni mwanachama wa muda mrefu wa Simba tunaelewa ni jinsi gani anaipenda Simba, asilimia zaidi ya 85 ya sisi wanachama wa Simba tunakubaliana na wazo la MO na tunajua ana nia ya kuisaidia Simba na hata soka la sasa limebadilika tofauti na zamani hivyo ni sahihi anavyotaka kufanya na mimi nitumie fulsa hii kumuomba MO abadilishe mawazo yake na aendelee kuwa na nia ya kuinunua Simba na sisi tupo nyuma yake,” alisema Mponda.
Aliongeza kuwa MO amekuwa mwanachama wa muda mrefu wa Simba na anatambua taratibu za Simba hivyo anapaswa kuwa na subira ili kabla ya klabu kufikia uamuzi wa kukubali kuiuza klabu, mashabiki wa Simba ambao katika katiba ya klabu hiyo ndiyo wanajulikana kama wamiliki wa klabu wanatakiwa kuzungumza kwa pamoja na kutoka na jibu moja juu ya kukubali au kukataa kuiuza timu yao.