Batuli azungumzia kurejea kwa tamthilia za mastaa wa Bongo, atoa ushauri huu

Muigizaji wa filamu nchini, Yobnesh Yussuf maarufu kama Batuli amesema yeye ni mmoja wa watu waliofurahi kuona kuwa waigizaji maarufu nchini wanarejea kwenye tamthilia.
12445799_868152293294128_1303469423_n
Miongoni mwa waigizaji wanaokuja na tamthilia zao ni JB, Irene Uwoya pamoja na Ray na Johari. Amesema kwa ulimwengu wa sasa tamthilia haziepukiki na ni muhimu Tanzania zikawepo nyingi pia.
“Huko nyuma filamu ndizo zilikuwa soko lenyewe lakini sasa hivi dunia inataka filamu lakini pia inataka tamthilia,” ameiambia Bongo5.
Amesema kuona wasanii wenzake wanakuja na tamthilia zao ni habari njema kwake kwasababu yeye ni mmoja wa watu waliochoka kuona tamthilia za nje ya nchi zikitawala runinga za nyumbani.
“Tumechoka kuona sijui kwa mfano Isidingo, kitu cha miaka na miaka mpaka waliogiza wengine walishakufa wengine tukiwa wadogo hadi tumekua. Kwahiyo ingependeza badala ya hizi series za kifilipino au nchi zingine basi zikakaa tamthilia zetu,” ameongeza.
“Nawapongeza wasanii wenzangu wote ambao wanafikiria au wapo katika process ya kufanya hicho kitu.”
Batuli pia ametaka wamiliki wa runinga za Tanzania kutoa nafasi kwa tamthilia za nyumbani. “Waweke uwiano kwamba hata kama wanaonesha za nje basi na za kwetu zipewe nafasi pia,” amesisitiza.
Hata hivyo Batuli amewashauri wasanii kuhakikisha wanatengeneza tamthilia ambazo zinaendana na mazingira ya Kitanzania.
“Waangalie kijamii zaidi, kitamaduni zaidi wasiigize sana kwa kuangalia mazingira ya nje ukiangalia haina tofauti na Isidingo kuanzia mavazi, uhalisia wanaishi maisha yao. Waigize vitu ambavyo vipo ili kushika soko kwasababu ili ushike soko hata kama utafanya tamthilia mia unaweza usishike soko. Zamani Kaole ilishika kwasababu vilivyokuwa vinaigizwa vipo kwenye jamii na vilikuwa kwenye mienendo ambayo baba atakaa ataangalia, mama ataangalia, watoto wataangalia. Kwahiyo wazingatie zaidi ili kutopotosha watoto kwasababu watakaokuwa wakiangalia tamthilia hizi ni watoto, wengi ni wasichana, wengine ni wavulana, teenagers, kwahiyo tamthilia zao ziangalie maadili ya kutowapoteza hawa wanaotazama.”
Hivi karibuni JB anatarajia kuja na tamthilia yake ya Kiu ya Kisasi anayooendelea kuitayarisha na Irene Uwoya anajiandaa kuja na yake iitwayo Drama Queen.

Post a Comment

Previous Post Next Post