Rais Magufuli Awapangia Vituo vya Kazi Mabalozi Watatu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu ambao aliwateua tarehe 03  Desemba 2016.
Mabalozi hao waliopangiwa vituo ni Joseph Sokoine anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Omar Yussuf Mzee anayekuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Algeria na Grace Mgavano anayekwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Ladis Komba nchini Uganda ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, Balozi Sokoine ambaye anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nafasi ya mwisho alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza ya Rais Dkt. Ali Mohammed Shein.
Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Ubalozi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.
Mabalozi wote waliopangiwa vituo vya kazi wataapishwa na Rais Ikulu jijini Dar Es Salaam leo  Jumapili tarehe 12 Februari 2017 saa tano asubuhi.

Post a Comment

Previous Post Next Post