Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu ambao
aliwateua tarehe 03 Desemba 2016.
Mabalozi hao waliopangiwa vituo ni Joseph Sokoine anayekuwa Balozi
wa Tanzania nchini Ubelgiji, Omar Yussuf Mzee anayekuwa Balozi wa kwanza
wa Tanzania nchini Algeria na Grace Mgavano anayekwenda kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Dkt. Ladis Komba nchini Uganda ambaye amestaafu kwa
mujibu wa Sheria.
Aidha, Balozi Sokoine ambaye anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa
wazi na Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya
Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo alishawahi
kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nafasi ya mwisho alikuwa
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza
ya Rais Dkt. Ali Mohammed Shein.
Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Ubalozi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.
Mabalozi wote waliopangiwa vituo vya kazi wataapishwa na Rais Ikulu
jijini Dar Es Salaam leo Jumapili tarehe 12 Februari 2017 saa tano
asubuhi.
إرسال تعليق