MJUE ABDALLAH SALIM JUMA, MTAMBO MPYA WA MABAO MSIMBAZI KUTOKA JESHINI

MJUE ABDALLAH SALIM JUMA, MTAMBO MPYA WA MABAO MSIMBAZI KUTOKA JESHINI



Na Dorris Maliyaga
FURAHA hukamilika kwa mchezaji yeyote anayetoka katika timu ndogo za Ligi Kuu Tanzania Bara na kujiunga na moja ya klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam.
Mshambuliaji Abdallah Salim Juma ni kati ya wachezaji wenye furaha msimu huu kwa sababu ataanza kuonekana katika jezi za rangi nyekundu na nyeupe.
Hii ni baada ya kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Ruvu Shooting na ataanza kuonekana katika klabu yake hiyo mpya kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Abdallah, ambaye ni mrefu kwa umbo na ana nguvu, sifa ambazo humfanya awe kikwazo kwa mabeki wasumbufu ambao huambulia patupu wanapojaribu kumdhibiti na ndicho kilichowashawishi mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kumsajili.
Kutokana na mafanikio hayo, Mwanaspoti ilimtafuta nyota huyo na kufanya naye mahojiano ya kina na yeye anaeleza sababu ya kutua hapo na malengo yake kwa ujumla.

Sababu ya kujiunga Simba 
Abdallah aling'ara akiwa na Ruvu Shooting msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kutokana na mchango wake hadi kuibakiza klabu hiyo katika ligi na ndiyo sababu iliyowavutia Simba wakamsajili.
Anasema amejiunga hapo kwa sababu yalikuwa malengo yake ya muda mrefu; "Nilikuwa na mipango ya kucheza klabu kubwa nisiishie hizi ndogo, ikiwa ni njia ya kufanikiwa mipango yangu kucheza soka la ushindani nje ya nchi.
"Hata hivyo, Simba naipenda, lakini pamoja na mapenzi yangu maslahi pia yamechangia, mimi ni mchezaji na kipaji changu cha soka ndiyo ajira yangu, kipato nitakachokipata hapa si sawa na nilichokuwa nakipata nikiwa na Ruvu,"anasema Abdallah, ambaye anaishabikia Arsenal ya England.
Anaeleza kuwa kutua kwake Simba ni hatua ya mafanikio makubwa kwake.
Abdallah amezungumzia pia changamoto na ushindani wa namba atakaokutana nao klabuni hapo; "Ushindani upo kila mahali na hasa katika klabu kubwa kama Simba, nimejipanga kuhakikisha nakabiliana nazo ili kuipa mafanikio klabu yangu,"anasema Abdallah, anayependa soka ya Fernando Torres wa Chelsea.
"Ninachowaahidi mashabiki wa Simba watulie na wanipe ushirikiano kwani nitajituma kadri niwezavyo nikishirikiana na wenzangu kuhakikisha tunaipa mafanikio Simba," anaongeza Athumani.

Fundi wa magari Abdallah anasema mbali na kipaji cha soka yeye ni fundi mzuri wa magari.
"Kabla sijaingia rasmi kwenye soka, nilipomaliza shule nyumbani Shinyanga, nilienda kwa dada yangu Sheila ambaye anaishi Simanjiro, Manyara, nilipokuwa huko alinisomesha Chuo cha Veta ambako nilisoma ufundi wa magari.
"Nilipata elimu hiyo na mara nyingine huwa nafanya kazi hiyo kwani naimudu vizuri,"anasema Abdallah ambaye anaweka wazi aliifanya kazi hiyo, alipokuwa anaichezea AFC Arusha.
"Nilikuwa nafanya shughuli ya ufundi magari kipindi cha mapumziko ya ligi au baada ya mechi, wakati huo nilikiwa naichezea AFC Arusha.
"Kuna gereji moja iko Ngaramtoni, Arusha ndiko nilikuwa naenda kufanya shughuli zangu huko,"anaeleza Abdallah.
Amefafanua kuwa tangu alipoondoka Arusha na kuja Dar es Salaam alipojiunga na Ruvu Shooting hakuweza kufanya tena shughuli hizo kutokana na kukosa muda.

Nje ya soka "Ninapokuwa sina majukumu ya soka, huwa napenda kutulia nyumbani kuangalia picha za Kihindi na msanii ninayempenda ni Akshey,"anasema Abdallah.
Ameweka wazi kuwa husikiliza pia muziki wa Bongo Fleva na msanii anayempenda ni Juma Nature.

Alikotokea Abdallah anasema, kipaji chake cha soka tangu alipokuwa mtoto mdogo akiwa shule ya msingi Buhangila alikosoma hadi la tatu kabla ya kuhamishiwa Salawe alikomaliza darasa la saba na zote ziko Shinyanga.
Alipata umaarufu zaidi alipokuwa akiichezea klabu yake ya mtaa ya Vijana Sejese, Kahama, Shinyanga na kushiriki michuano mbalimbali.
"Hapo niling'ara na ndio Polisi Shinyanga waliniona na kunisajili kabla ya kujiunga na Mwanza United," anaeleza Abdalah ambaye hata hivyo hakudumu na Mwanza United na kusajiliwa na AFC Arusha mwaka 2007.
Anasema aliichezea AFC kwa msimu mmoja akaenda Kagera Sugar na kuichezea misimu miwili, baada ya hapo alirudi tena AFC Arusha mwaka 2010 wakaipandisha Ligi Kuu na mwaka 2011 alitua Ruvu Shooting na sasa Simba.

Historia Abdallah anasema katika familia yao walizaliwa watatu, lakini mkubwa wao, Sadi ni marehemu na yeye ni wa mwisho yupo na kaka yake, Juma.
Alisoma na Shule ya Msingi ya Buhangija, Shinyanga na kumalizia darasa la saba Salawe kabla ya kujiunga na Chuo cha Veta huko Simanjiro.
Upande wake, yeye ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa, Salum (2) na mke mmoja anaitwa, Amina Yusuph.

SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI

Post a Comment

أحدث أقدم