KONGAMANO LA MICHEZO KWA MAENDELEO NA AMANI KUANZA KESHO.
Na Mwandishi wetu
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na taasisi za
Right To Play na British Council zimeandaa Kongamano la Michezo kwa
Maendeleo na Amani linalotarajia kuanza kesho katika Hoteli ya Blue Pearl kuanzia 3: 00 asubuhi.
Akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Bw. Leonard Thadeo amesema lengo
kubwa la Kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali
kubadilishana mawazo, kupeana uzoefu na kuangalia kwa pamoja changamoto
zinazoikabili sekta ya michezo nchini.
Bw. Thadeo amesema, katika Kongamano
hilo washiriki wataangalia Sera ya Michezo inazungumziaje matumizi ya
michezo kama nyenzo ya kukuza maendeleo na kuhamasisha amani.
Aidha, amesema kutakuwa na mjadala wa
kuangalia ni jinsi gani michezo inaweza kusaidia utekelezaji wa
Mikakati mbalimbali ya kitaifa kama vile MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa
Maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Right To Play nchini, Bibi Josephine Mukakalisa amesema michezo
inatumika si tu kuburudisha bali pia kuelimisha, kuhamasisha watoto wa
jinsia zote kushiriki katika uongozi na kutoa maamuzi yanayolenga
kuendeleza jamii husika.
Kwa upande wake Meneja Mradi, British
Council, Bw. George Agango ameeleza kuwa Kongamano hilo ni fursa kwa
wadau kujadili kwa pamoja namna ya kuendeleza vijana katika michezo na
kuhamasisha watoto wa kike na walemavu kushiriki katika michezo kwa
ajili ya Maendeleo.
Kongamano hilo
la siku mbili litashirikisha Vyama vya Michezo, Wawakilishi wa Mikoa,
Ofisi za Kibalozi nchini, Ofisi za Serikali na Wanahabari.
إرسال تعليق