Na Majid Ahmed, Mogadishu
Amri ya al-Shabaab kuyapiga marufuku mashirika ya msaada ya kiutu katika
maeneo inayoyadhibiti kunazidisha mgogoro wa kibinaadamu nchini Somalia
na kuhatarisha maisha ya maelfu ya wahanga wa njaa, wasema maafisa wa
serikali na wafanyakazi wa msaada.
Tarehe 8 Oktoba, al-Shabaab ililipiga marufuku shirika la msaada la
Islamic Relief la Uingereza kufanya kazi zake katika maeneo yaliyo chini
ya udhibiti wake, ikililaumu shirika hilo kwa kufanya kazi kwa siri na
mashirika ya msaada ambayo kundi hilo ilishayafukuza. Shirika la Islamic
Relief limekuwa likifanya kazi nchini Somalia tangu mwaka 2006.
"Islamic Relief imeshindwa mara kadhaa, licha ya onyo la mara kwa mara,
kuheshimu miongozo ya kufanya kazi iliyowekwa na OSAFA (Ofisi ya
al-Shabaab ya Kusimamia Masuala ya Mashirika ya Msaada)," al-Shabaab
ilituma taarifa yake kwenye Twitter. "Islamic Relief pia iligundulika
kutanua huduma zake kwa siri kwa mashirika yaliyopigwa marufuku, hasa
WFP (Shirika la Mpango wa Chakula Duniani), katika maeneo yaliyo chini
ya HSM [Harakat al-Shabaab al-Mujahideen]."
Islamic Relief ilikana tuhuma hizo. "Hakuna hata programu yetu moja
nchini Somalia inayofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani,"
alisema Iftikhar Shaheen, mkurugenzi wa shirika hilo kwa kanda ya Afrika
ya Mashariki, katika taarifa yake. "Ikiwa uamuzi huu utathibitishwa,
utayatia hatarini maisha ya watu wengi, kuhatarisha kazi yetu ya kutoa
chakula, maji, huduma za usafi na tiba na msaada kwa ajili ya kuongeza
kipato kwa watu milioni 1.3 nchini Somalia."
Mnamo mwaka 2010, al-Shabaab pia ililipiga marufuku shirika la Mpango wa
Chakula Duniani, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Idara ya
Umoja wa Mataifa ya Usalama, shirika la kimataifa la Mercy, shirika la
kimataifa la Oxfam, Shirika la Maendeleo la Italia, shirika la Msaada la
Kiislamu na shirika la Kimataifa la Care.
Serikali ya Somalia imelaani hatua hiyo ya al-Shabaab. "Uamuzi wa
al-Shabaab kuyafukuza mashirika ya kibinaadamu kutoka maeneo
inayoyadhibiti unayatia hatarini mamia kwa maelfu ya maisha ya watu,
hasa wanawake na watoto," alisema Abdullahi Jimale, mkuu wa Shirika la
Taifa la Kupambana na Majanga.
"Amri hii ya al-Shabaab ya kupiga marufuku mashirika ya msaada
yanaifanya hali ya kibinaadamu kuwa mbaya zaidi na kuyafanya maisha ya
watu kuzidi kuwa magumu," aliiambia Sabahi. "Tunawatolea wito al-Shabaab
kujiepusha na kuweka siasa kwenye masuala ya msaada ya kibinaadamu,
inayokusudiwa kuyanusuru maelfu ya maisha ya watu wenye uhitaji mkubwa."
Jimale aliitaka al-Shabaab kuyaruhusu mashirika ya msaada ya ndani na ya
kimataifa yanayotaka kuwasaidia watu wa Somalia kufanya kazi katika
maeneo yote kuwanusuru wale walioathirika. Pia aliyaomba mashirika ya
msaada kutoa msaada wa haraka katika maeneo mapya yaliyokombolewa kama
vile Kismayu, Marka na Wanlaweyn, na pia katika sehemu za Beledweyne
zilizoathiriwa na mafuriko ya hivi karibuni.
Kufukuzwa kwa mashirika ya msaada za Kiislamu kwawaua njaa wahanga wa ukame
Abdifatah Mohamed, mkurugenzi wa operesheni wa Badbaado, ambalo ni
shirika la msaada na maendeleo nchini Somalia, alisema al-Shabaab
wanaifanya hali ya kibinaadamu nchini Somalia kuwa mbaya zaidi kwa
sababu ya amri yake ya kupiga marufuku mashirika ya msaada ya kimataifa.
"Al-Shabaab ndiyo inayobeba dhamana ya kuzorota kwa hali ya kibinaadamu
nchini Somalia kwa sababu inazuia upitishaji wa msaada kwa maeneo
yaliyoathirika," Mohamed aliiambia Sabahi.
Mohamed alisema kwa al-Shabaab kuyafukuza mashirika ya msaada inakusuda
kuwafanya watu wafe njaa, hasa wahanga wa ukame. "Hapo zamani,
al-Shabaab iliyapiga marufuku mashirika ya msaada yasiyo ya Kiislamu
kufanya kazi kwa sababu ilidai mashirika hayo yangelifanya shughuli za
kutia mashaka zaidi ya zile za kibinaadamu. Ujanja huo, hata hivyo,
haufanyi tena kazi baada ya kundi hilo kuifukuza Islamic Relief,"
alisema.
"Imekuwa wazi kwamba al-Shabaab haina huruma yoyote kwa wahanga wa
ukame, kwani imezuia chakula na madawa kuwafikia na imeyafukuza
mashirika ya msaada yaliyokuja Somalia kuwasaidia Wasomalia walio kwenye
hali ngumu," alisema Mohamed.
"Pamoja na yote hayo, al-Shabaab inaweka vikwazo vya kikatili dhidi ya
raia wanaoishi kwenye maeneo inayoyashikilia katika kiwango ambacho
inawazuia wenye uhitaji mkubwa kwenda kwenye kambi za msaada katika
maeneo yanayodhibitiwa na serikali," alisema. "Huu ni ushahidi kwamba
al-Shabaab haina ubinaadamu na haina hisia za kiutu inapowashughulikia
wahanga wa ukame."
Maonyo ya uhaba wa chakula wa mara kwa mara
Ahmed Sheikh Muse, anayefanya kazi na Sardo ambalo ni shirika la ndani
la msaada, alisema hali ya kibinaadamu nchini Somalia itazorota baada ya
kufukuzwa kwa mashirika ya msaada ya kimataifa.
"Mavuno ya msimu uliopita yalikuwa madogo, hali iliyosababisha kupanda
kwa bei za nafaka na chakula. Hili linawalazimisha watu wengi zaidi
kutegemea chakula cha msaada, lakini amri ya al-Shabaab kupiga marufuku
mashirika ya msaada katika maeneo inayoyadhibiti inafanya mambo kuwa
mabaya zaidi," aliiambia Sabahi.
Kwa mujibu wa utafiti mpya wa shirika la kimataifa la Oxfam, upungufu wa
chakula na maji katika baadhi ya sehemu za Somalia umefikia kiwango cha
kutisha, pamoja na kupanda sana kwa idadi ya walio na utapiamlo, hasa
katika mikoa ya Gedo, Bakool na Lower Jubba. Hata hivyo, Oxfam inasema
kurudi tena kwa ukame ni jambo lisilotarajiwa.
"Kimbunga kikali cha msimu mbaya wa mvua uliopita, kushindwa kukua kwa
mazao, kufa kwa wanyama na kukosekana kwa usalama kunamaanisha kwamba
watu waliokuwa wameanza kujishika mwaka jana, sasa wanategemea msaada
kwa kiasi kikubwa," alisema mkurugenzi wa Oxfam nchini Somalia, Senait
Gebregziabher.
Oxfam ilifanya uchunguzi wa maoni ya watu kwa familia 1,800 katika
maeneo 40 kwenye maeneo ya kati na kusini mwa Somalia mwezi wa Julai na
Agosti ili kujua athari za ukame ulioikumba Somalia mwaka jana na
kusababisha njaa iliyogharimu maisha ya maelfu ya watu. Oxfam iligundua
kwamba asilimia 72 ya washiriki wa uchunguzi huo wa maoni wanahofia
kwamba hakutakuwa na chakula cha kutosha kwa miezi minne ijayo, wakati
asilimia 42 walisema walilazimika kuruka baadhi ya mlo
إرسال تعليق