MADRID, Hispania
KUAMUA nani wa kutomuanzisha kikosini ndiko kunakoonekana kuwa tatizo kubwa kwa kocha Vicente del Bosque wa timu ya taifa ya Hispania wakati watakaposhuka dimbani jijini Madrid leo kucheza dhidi ya Ufaransa katika mechi yao ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Mabingwa hao wa Dunia na Ulaya wamekuwa na tatizo la kuwa na nyota wengi walio tayari kucheza na hivyo haitakuwa ajabu ikiwa Del Bosque hatajua nani wa kuwaanzisha katika kikosi chake bora cha kwanza dhidi ya vinara wenzao wa Kundi I.
Kocha huyo mwenye miaka 61 alifanya mabadiliko ya kushangaza katika mechi yao ya ugenini Ijumaa dhidi ya Belarus, akimchezesha kiungo Sergio Busquets katika nafasi ya beki wa kati, na kumpa Santi Cazorla nafasi ya kuanza kikosini baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika miezi miwili iliyopita kwenye kikosi cha klabu yake mpya ya Arsenal.
Kikosi hicho kilichobadilishwa kilipata ushindi mnono wa 4-0 huku Pedro aliyekuwa katika kiwango chake cha juu 'akitengeneza' goli moja na kufunga mengine matatu (hat-trick), akimfanya mfungaji mwenye mabao mengi kuliko wote katika historia ya Hispania, David Villa acheze kwa dakika 15 tu baada ya kuingia akitokea benchi. Fernando Torres hakupata nafasi kabisa.
Andres Iniesta huenda akapangwa leo, kama ilivyo kwa beki halisi wa kati, Raul Albiol, wakati Hispania ikisaka ushindi wake wa 25 mfululizo katika mechi za awali za kuwania kufuzu kwa fainali za michuano mikubwa.
"Tuna bahati ya kuwa na wachezaji wengi wanaoweza kucheza nafasi nyingi uwanjani," mshambuliaji wa Barcelona, Pedro aliuambia mkutano na waandishi wa habari juzi.
"Tuko wazi na dhana na falsafa yetu ya kucheza, yeyote anaweza kupangwa na kucheza vizuri, na hilo haliwezi kuathiri uchezaji wa timu ya taifa."
Hispania, waliowafunga Ufaransa 2-0 katika robo fainali kabla ya kutwaa ubingwa wa Euro 2012, wanaongoza Kundi I kwa tofauti ya magoli dhidi ya wapinzani wao wa leo baada ya wote kushinda katika mechi zao mbili za ufunguzi.
Huku timu moja tu katika kundi ikiwa na uhakika wa kufuzu moja kwa moja kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil 2014, vita iliyopo ni kwa timu hizo zinazopewa nafasi kubwa ya kuongoza kundi kuepuka kumaliza katika nafasi ya pili na kulazimika kucheza hatua ya mtoano ili kuwania nafasi ya kufuzu.
KIPIGO CHA KWANZA
Ufaransa watashuka dimbani leo wakiwa na kumbukumbu ya kupata kipigo chao cha kwanza tangu waanze kuongozwa na Didier Deschamps aliyerithi mikoba ya Laurent Blanc baada ya fainali za Euro 2012, wakilala 1-0 katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki waliyocheza Ijumaa dhidi ya Japan kwenye uwanja wa Stade de France.
Kwa mara nyingine tena, mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema, ambaye amefunga magoli 15 katika mechi 53 alizoichezea Ufaransa, alishindwa kutikisa wavu.
Viungo walishindwa kumiliki mchezo na mabeki walionekana kuyumba, hasa katika nafasi za pembeni.
Huku Abou Diaby na Rio Mavuba wakiwa majeruhi, Deschamps pia atalazimika kupanga kikosi kisichokuwa na viungo wake wakabaji wa kikosi cha kwanza.
Taarifa mbaya zaidi kwake ni kukosekana kwa kiungo mkabaji aliye katika kiwango cha juu wa klabu ya Paris St Germain, Clement Chantome aliyejiondoa kikosini Ijumaa baada ya kuumia.
"Itakuwa vizuri kuifanyia Hispania kile ambacho Japan walitufanyia sisi," alisema mshambuliaji Olivier Giroud.
Ufaransa walifungwa kwa shambulizi la kustukiza dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.
"Tutakuwa na nafasi chache dhidi ya Hispania lakini tutapaswa kuzitumia vizuri," alisema winga Mathieu Valbuena.
Vikosi vinavyotarajiwa kuanza LEO:
Hispania:
Iker Casillas; Alvaro Arbeloa, Sergio Ramos, Raul Albiol, Jordi Alba; Sergio Busquets, Xabi Alonso, Pedro, Xavi, Andres Iniesta na Cesc Fabregas
Ufaransa:
Hugo Lloris; Mathieu Debuchy, Laurent Koscielny, Mamadou Sakho, Patrice Evra; Moussa Sissoko, Yohan Cabaye, Blaise Matuidi; Franck Ribery, Karim Benzema na Jeremy Menez.
RATIBA MECHI ZA KOMBE LA DUNIA
LEO, Jumanne
Hispania v Ufaransa (saa 5:00) usiku
Ujerumani v Sweden (saa 4:45) usiku
Italia v Denmark (saa 4:45) usiku
Poland v England (saa 5:00) usiku
Romania v Uholanzi (saa 4:00) usiku
Ureno v Ireland (saa 5:45) usiku
MECHI YA KIRAFIKI
Japan V Brazil (saa 10:10) jioni
MECHI NYINGINE ZA LEO
Croatia V Wales (saa 4:00) usiku
Macedonia V Serbia (saa 4:30) usiku
Ubelgiji V Scotland (saa 4:45) usiku
Jamhuri ya Czech V Bulgaria (saa 4:00) usiku
Visiwa vya Faroe V Ireland (saa 4:00) usiku
Austria V Kazakhstan (saa 4:35) usiku
Andorra V Estonia (saa 3:00) usiku
Hungary V Uturuki (saa 4:30) usiku
Cyprus V Norway (saa 3:00) usiku
Iceland V Uswisi (saa 4:30) usiku
Albania V Slovenia (saa 4:45) usiku
Urusi V Azerbaijan (saa 1:00) usiku
Israel V Luxembourg (saa 2:00) usiku
Latvia V Liechtenstein (saa 3:00) usiku
Bosnia V Lithuania (saa 4:00) usiku
Slovakia V Greece (saa 4:30) usiku
Ukraine V Montenegro (saa 4:00) usiku
San Marino V Moldova (saa 4:30) usiku
Belarus V Georgia (saa 2:00) usiku
إرسال تعليق