MAUAJI YA RPC BARLOW SIMU ZACHUNGUZWA

Na Mwandishi Wetu
UTATA bado umegubika mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliyepoteza maisha kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa Oktoba 12 mwaka huu, Uwazi limejuzwa.
Taarifa kutoka chanzo chetu cha kuaminika zinaeleza kuwa tayari polisi wameingia kazini kuchunguza sababu hasa za mauaji hayo na waliohusika huku simu alizopigiwa na alizopokea kamanda huyo wiki moja kabla ya mauaji zikifuatiliwa kwa kina.

Afande George Msangi akiongoza ratiba za kumuaga aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Liberatus Barlow aliyeuawa usiku wa kuamkia Jumamosi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi.
Aidha, chanzo hicho cha ndani ya jeshi kikasema kuwa polisi wataenda kwa mtu mmoja mmoja kufuatilia hata uhusiano na ukaribu wake na marehemu, kwa maana hiyo hata mwalimu Doroth Moses wa Shule ya Msingi Nyamagana jijini Mwanza ambaye siku ya tukio alikuwa na marehemu simu yake itachunguzwa.
“Polisi wameingia mpaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na katika mitandao mbalimbali ya simu ili kuchunguza mawasiliano ya Kamanda Barlow na watu wengine.

                     Mwili wa Marehemu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow ukiagwa katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
 “Polisi kwa sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina na wanaamini kuchunguza simu pamoja na msaada kutoka kwa wasamaria wema ni mambo ambayo yanaweza kuwasaidia kuwabaini wauaji,” kilisema chanzo chetu na kuongeza kuwa kitendo cha wauaji kuchukua vitu kadhaa vya marehemu ikiwemo bastola na simu zake za mkononi  kumewavuruga zaidi polisi.
Kamanda Barlow aliyekuwa akiendesha gari lake binafsi aina ya Toyota Hilux- Double Cabin baada ya kuuawa habari zinasema wauaji walichukua simu zake mbili, ambazo sasa polisi wanazifanyia kazi kwenye mitandao ya simu.
Habari za ndani za kipolisi zinasema kuwa mwalimu Doroth ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mwanza kwa mahojiano zaidi tayari simu yake ipo mikononi mwa jeshi hilo kwa lengo lilelile la kuifanyia uchunguzi.
Bado wananchi wengi wa Mwanza wanaamini kwamba mtandao wa ujambazi ndiyo unahusika na kifo cha Kamanda Barlow kwa kuwa alikomaa nao kuhakikisha wahalifu hao hawafurukuti.

 Maofisa wa Polisi wakitoa saluti kwa Marehemu Kamanda wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow wakati akiagwa katika uwanja wa Namagana jijini Mwanza.
Mbali na mtandao wa ujambazi kutajwa, vibaka nao jijini humo wamekuwa na wasiwasi mkubwa, wanaishi kwa tahadhari wakiamini msako wa polisi wa safari hii utawaingiza selo wengi wao.
Kufuatia mauaji hayo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Robert Manumba ameweka kambi jijini Mwanza kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Manumba alipotafutwa na mwandishi wetu juzi Jumapili na kuulizwa walichokipata kuhusiana na sakata hilo, alisema kwa kifupi kwamba waachwe wafanye upelelezi wao na watatoa taarifa kwa wana habari wakati muafaka ukifika.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumzia mauaji hayo walielezea kushangazwa kwao na hatua ya Barlow kutembea usiku bila mlinzi wake (bodyguard) ambaye kwa kiwango kikubwa angeweza kusaidia kumuepushia kifo hicho.

 Wanafamilia wa marehemu, Kamanda Liberatus Barlow wakiwa na majonzi makubwa sana katika uwanja wa Nyamagana wakati wa kuuaga mwili wa mpendwa wao.
Aidha, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, katika taarifa aliyoitoa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema ameshamtuma DCI  Manumba kuimarisha ulinzi na upelelezi wa tukio hilo na amewaomba wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo utakaowezesha kuwabaini wauaji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alipoongea na wana habari mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema mauaji hayo yalifanyika kati ya saa 7 na saa 8 usiku, wakati Barlow akimsindikiza mwalimu Doroth.
Inasemekana wote wawili walikuwa wametoka kuhudhuria kikao cha maandalizi ya harusi ya mtoto wa dada wa Barlow, kilichofanyika kwenye Hoteli ya Florida jijini Mwanza.
Marehemu Lebaratus Barlow anakuwa kamanda wa polisi wa kwanza nchini kuuawa. Miaka ya sabini, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kleruu naye aliuawa lakini mauaji yake yalitekelezwa na mkulima aliyeitwa Said Mwamwindi kufuatia madai ya kutofautiana ‘lugha’.

GPL

Post a Comment

أحدث أقدم