Rais Obama amekuja juu katika mdahalo wa
pili wa wagombea urais nchini Marekani, na kumshambulia mpinzani wake
Mitt Romney wa chama cha Republican kuhusu mashambulizi ya Ubalozi
nchini Libya na pia biashara zake.
Obama ameonekana kuzinduka kutokana na jinamizi lililomfanya aonekane
mnyonge katika mdahalo wa kwanza uliofanyika mjini Denver mwezi
uliopita, na maoni ya wachambuzi wengi ni kwamba ametawala jukwaa katika
mdahalo wa pili, ambao umemalizika alfajiri ya leo ( 17.10.2012) kwa
saa za Afrika ya mashariki.
Kura za maoni zilizochapishwa na kituo cha televisheni cha CNN ambacho
kimeendesha mdahalo huo, zimeonyesha kwamba Rais Obama ameibuka kifua
mbele dhidi ya Gavana Romney ambaye ametetereka.
Mdahalo ulikuwa mkali, wagombea wakikabiliana ana kwa ana na
kubadilishana maneno makali, huku kila mmoja akinuia kumuonyesha
mpinzani wake kama mtu asiyefaa kuiongoza Marekani.
Kutoana kimasomaso
Rais Obama na Gavana Romney, wakirushiana cheche wakati wa mdahalo
Rais Obama alimuangalia usoni na kumnyoshea kidole Romney, akijibu
tuhuma za mgombea huyo wa chama cha Republican kwamba Obama na utawala
wake walishindwa kuchukua hatua mwafaka kukabiliana na mashambulizi
kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya, ambayo yalimuuwa
balozi na raia wengine wanne wa Marekani.
''Madai yoyote kwamba mtu yeyote katika timu yangu, iwe waziri wa mambo
ya nchi za nje, au balozi kwenye Umoja wa Mataifa, anaweza kutumia vifo
vya watu wetu wanne kisiasa, ni uchokozi. Hayo siyo tunayofanya, hayo
siyo ninayoyafanya kama rais na jemadari wa majeshi''. Alisema kwa ukali
rais Obama.
Wa-Republican walitaka kuyatumia mashambulizi ya Benghazi kuzitia doa sifa alizopata Rais Obama katika masuala ya usalama na sera za nchi za nje.
Romney alijaribu kujipanga upya kwa kumshutumu Obama kutosema kwa wakati
unaofaa kwamba mashambulizi yale yalikuwa tendo la kigaidi, lakini
Obama alimpa changamoto ya kusoma hotuba aliyoitoa mara tu baada ya
mashambulizi, na aliungwa mkono na mwongozaji wa mdahalo, Candy Crowly.
Romney ajibu mapigo
Wakati ambapo Romney alimbana pumzi rais Obama ni pale alipotoa shutuma
kali akielezea jinsi rais huyo alivyoshindwa kufufua uchumi na kuunda
nafasi za kazi kama alivyoahidi wakati aliposhinda muhula wa kwanza wa
miaka minne.
Romney alisema, ''Alipochukua madaraka asilimia 7.8 ya wamarekani
hawakuwa na ajira, wasio kuwa na ajira leo hii ni hao hao asilimia 7.8,
lakini ukitilia maanani watu walitoka katika kundi la wafanyakazi,
itakuwa asilimia 10.7. Hatujawa na maendeleo yanayowezesha kuwarudisha
watu kazini''
Ahueni kwa upande wa Obama
Wachambuzi wanasema matokeo ya mdahalo wa leo yatawakatisha tamaa wa
Republican ambao walitaka mgombea wao ammalize kabisa rais Obama, na kwa
upande mwingine utashangiliwa na wa Democrats ambao wanaamini kwamba
mgombea wao amepata msukumo mpya.
John Pitney ambaye ni profesa wa masomo ya siasa kwenye chuo kikuu cha
Claremont McKenna, amesema usiku wa leo ulikuwa bora kwa Obama,
ukilinganishwa na ule wa mjini Denver.
Mdahalo huu umefanyika zikisalia wiki tatu tu kabla ya uchaguzi wa mwezi
Novemba. Mdahalo wa tatu na wa mwisho utafanyika tarehe 22 mwezi huu
huko Boica Raton, Florida.
إرسال تعليق