SIMBA jana ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na kombaini ya Polisi katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilikuwa ya kujipima nguvu kwa Simba kabla ya kuanza kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyopangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.
Nayo kombaini ya Polisi ililitumia pambano hili kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya SADC inayotarajiwa kuanza Agosti 18 mwaka huu nchini Namibia.
Katika mechi hiyo, Simba iliwatumia wachezaji wake wengi wapya waliosajiliwa msimu huu, akiwemo kiungo Abdulrahim Humud kutoka Azam na mshambuliaji Betram Mwombeki, ambaye alikuwa akiishi Marekani.
Mwombeki ndiye aliyeifungia Simba bao la kuongoza na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0. Alifunga bao hilo dakika ya 17 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Sino Agustino.
Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Abdalla Kibadeni wa Simba katika kipindi cha pili yaliidhoofisha timu hiyo, hasa katika safu ya kiungo na kuifanya Polisi kutawala.
Bao la kusawazisha la Polisi lilifungwa na Nicilas Kapibe dakika ya 60 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na mkongwe Bantu Admini.
إرسال تعليق