Tigo yatoa rai kwa wakulima kutumia huduma ya ‘Tigo Kilimo’.


2
Meneja wa mradi wa Tigo Kilimo Bw. Yaya  Ndjore (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari  (hawapo pichani) mkoani Dodoma kuelezea mikakati walionayo kuwawezesha wakulima nchini kwa kujiunga na huduma hiyo ya Tigo Kilimo ili kupata taarifa mbalimbali za kilimo ikiwemo mbinu bora za kilimo, hali ya hewa na bei za mazao. Pembeni yake ni Meneja Biashara wa Tigo mkoa wa Dodoma Bw. Saitoti Naikara.
Tigo Tanzania imetoa rai kwa wakulima zaidi nchini kuchangamkia huduma ya simu “Tigo Kilimo” kama namna ya kupata taarifa za kilimo ambazo zitawawezesha kuzalisha zaidi na kupata taarifa bora za masoko kwa ajili ya kuuza bidhaa zao kwa bei ya faida.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tigo katika Sikukuu ya Wakulima ‘Nane Nane’ itakayofanyika jijini Dodoma wiki ijayo, Meneja Mradi wa Tigo Kilimo, Bw. Yaya Ndjore alisema kwamba tayari Tigo imetoa teknolojia ya simu ya kisasa katika huduma ya kilimo ambayo inahusu kifurushi maalum inayojumuisha namna bora ya kufanya kilimo, bei za masoko kwa bidhaa za kilimo, pamoja na utabiri wa hali ya hewa.
“Toka tuzindue huduma hii mwaka jana, kundi kubwa la wateja wetu kutoka kila kona ya nchi wameweza kufaidika. Kwa maana hiyo tunapenda kuwaasa pia wakulima wengi zaidi kujiunga na huduma hii ya Tigo Kilimo kwa ajili ya kupata matokeo bora zaidi katika shughuli zao,” aliongeza Yaya.
“Tigo inajivunia kuwa kampuni ya simu ya kwanza kutoa huduma za taarifa za kilimo nchini Tanzania kupitia teknolojia ya simu za mkononi, ambayo inaendana sambamba na utamaduni wetu wa ubunifu ambayo Tigo inapenda kuonesha kila siku. Hakika majaribio ya teknolojia hii yamewapatia mafanikio makubwa kwa wakulima ambao wamefaidi taarifa za uhakika kuhusu mambo ya kilimo,” alisema Yaya.
Kutokana na Yaya, Tigo inawahudumia wakulima kupitia meseji (SMS) kwa kutoa taarifa za bei ya soko, utabiri wa hali ya hewa na namna bora ya kuendesha kilimo kwa mazao yanaongoza kulimwa nchini kwa mfano mpunga, mahindi, viazi mviringo na viazi vitamu, kwa kutaja machache.   
“Wakulima wana nafasi kubwa ya kufaidi huduma zetu si tu kwa sababu ya mtandao wetu mpana wenye uwezo wa kumfikia kila mkulima nchini aliyejisajili, bali pia kwa sababu mkulima hahitaji kulipia chochote kujisajili na kuingia katika huduma hii, pamoja na hayo kupata muhtasari wa taarifa ni bure pia,” aliongeza Yaya.
Kwa kuongezea, wakulima pia wanaweza kupata huduma za vifurushi vya wiki ambazo hazina kikomo katika idadi ya taarifa wanazoweza kupata, hii inamwezesha mkulima kupata huduma hii bila vikwazo vyovyote.    
Kuhakikisha kwamba tunawapatia huduma bora wakulima katika mikoa yote nchini, Tigo pia imeanza mkakati wa kuwa karibu na wateja wake kwa kuongeza ubora wa minara na mtandao wake mikoani. Huduma hii ya “Tigo Kilimo” inapatikana kwa kuingiza *148*14# katika simu aina yoyote ya mkononi yenye laini ya simu ya Tigo.

Post a Comment

Previous Post Next Post