Waziri wa zamani mahakamani kwa ufisadi Kenya

Waziri wa zamani wa ardhi Amos Kimunya
Waziri wa zamani katika serikali nchini Kenya, Amos Kimunya amefikishwa mahakamani mjini Nairobi kwa makosa ya kutumia vibaya mamlaka pamoja na kujipatia ardhi ya umma kinyume na sheria.
Waziri huyo wa zamani wa Ardhi, aliwasili mahakamani hapo jana kujibu mashitaka.
Bwana Kimunya pamoja na washitakiwa wenza ambao afisaa mmoja wa ardhi na afisaa wa kampuni inayomilikiwa na Kimunya, walifikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi kujibu mashitaka saba ya utumizi mbaya wa mamlaka na kujipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu.
Mwendesha mkuu wa mashitaka Keriako Tobiko, anadai kuwa bwana Kimunya alipokuwa waziri wa ardhi, akishirikiana na afisaa mmoja wa ardhi walitumia mbinu ya udanganyifu kuipatia kampuni moja inayomilikiwa na Kimunya , ardhi yenye thamani ya shilingi milioni sitini.
Kimunya pia alifahamishwa na mahakama kuwa alifanya kitendo hicho bila ya kujulisha serikali kuwa alikuwa afisaa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo.
Vile vile alishitakiwa kwa kosa la kukosa kulinda ardhi ya umma.
Kimunya na washitakiwa wenza wamekanusha mashitaka dhidi yao.
Alipokuwa waziri chini ya serikali ya Rais wa zamani Mwai Kibaki, Kimunya pia alihusishwa na sakata ya kuuza moja ya hoteli za kifahari nchini Kenya Grand Regency kwa kampuni ambayo alikuwa mkurugenzi wake.
- Bbc-

Post a Comment

أحدث أقدم