Jeshi la Polisi mkoani Mara limesema
kuwa linakamilisha taratibu za kisheria, ili liweze kumfikisha mahakamani
mtuhumiwa wa mauaji, anayedaiwa kuua mwenzake kwa kumpiga na rungu wakiwa kwa
mpenzi wao, ambaye wamekuwa wakifanya naye mapenzi kwa pamoja.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara,
Ferdinand Mtui alisema jana kuwa jeshi hilo linakamilisha taratibu za kisheria
ili kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Mtui aliwaondoa wasiwasi wanafamilia
ya marehemu Chacha Silasi, aliyeuawa kwa kupigwa na rungu na mtuhumiwa huyo,
Boniphace Wankuru Magabe, ambaye alidai walikuwa wakifanya mapenzi wote kwa
pamoja na mke wa mtu.
Alisema kuwa baada ya taratibu hizo
kukamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Baada ya taratibu kukamilika tutamfikisha
Mahakamani….lakini pia ndugu wa marehemu watupe ushirikiano, hasa wale
walioshuhudia mtuhumiwa akimshambulia marehemu,” alisema.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumpiga kwa
rungu mwenzake Februari 6, mwaka huu usiku katika Kijiji cha Wegero wilayani
Butiama, na kusababisha kifo chake Februari 8, akiwa katika Hospitali ya Mkoa
wa Mara, alikokimbizwa kwa matibabu.
Polisi walisema baada ya mtuhumiwa
huyo kufanya tukio hilo, alitoroka, lakini alikamatwa Machi 31, mwaka huu.
Aliachiwa kwa dhamana Aprili 23, akiwa katika Kituo cha Polisi Butiama.
Ilidaiwa kuwa baada ya kuachiwa,
alikwenda kijijini kwake na kutambia ndugu wa marehemu kwamba hawezi kufungwa
wakati akiwa na fedha, hali ambayo ilifanya wanafamilia hao kulalamika na
ndipo akakamatwa tena Aprili 28, mwaka huu.
Aidha, wanafamilia hao walidai kuwa
licha ya kukamatwa tena, mtuhumiwa huyo hajafikishwa mahakamani na bado yupo
katika Kituo cha Polisi Butiama, jambo ambalo linawatia shaka kwamba kuna
mchezo mchafu unataka kuchezwa.
Hata hivyo,
Mtui alisema mtuhumiwa huyo bado anafanyiwa mahojiano zaidi, ikiwa ni pamoja na
kukamilisha taratibu za kisheria ili aweze kufikishwa mahakamani.
إرسال تعليق