Fufa yamkwamisha Okwi Uganda

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.
Na Nicodemus Jonas
SHIRIKISHO la Soka Uganda (Fufa), limetajwa kuwa chanzo kikuu cha kuchelewa kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, kuungana na wenzake kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo nchini Afrika Kusini, kufuatia kushindwa kutuma barua rasmi kuhusiana na kuachwa kwa mchezaji huyo.
Okwi, aliitwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa, The Cranes, kilichomenyana na Togo Jumamosi iliyopita katika michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika, hata hivyo, baadaye alitemwa kwenye kikosi cha Kocha Milutin Sredojević   ‘Micho’ kitakachoivaa tena Togo leo.
Mpaka jana, Okwi ndiye mchezaji wa Simba, ambaye alikuwa hajafika kambini, baada ya wale wa Taifa Stars kuungana na wenzao juzi Jumatatu.Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa Simba, Humprey Nyasio, alisema kuwa mpaka jana Okwi alikuwa nchini Uganda.
“Okwi bado hajafika kambini kuungana na wenzake na sisi tunamfanyia taratibu zote ili kati ya leo (jana) au kesho (leo) aweze kuungana na wenzake.
“Kikubwa kinachokwamisha ni kwamba tumepata taarifa za kutemwa kwenye timu ya taifa, lakini hazijaja rasmi, kwa hiyo sisi tunasubiria barua kutoka kwa shirikisho la nchini mwao kuhusiana na kuondolewa kwake na muda wowote baada ya kupata taarifa rasmi tutamfanyia taratibu haraka iwezekanavyo ili aondoke,” alisema Nyasio na kuongeza kuwa huenda nyota huyo wa zamani wa Yanga akapitia hukohuko Uganda.
Iwapo taratibu hizo  zitakamilika leo, ina maana Okwi atajiunga na wenzake kwa siku moja ya Alhamisi kabla ya kikosi hicho kurejea Ijumaa, tayari kwa mchezo na watani wao Yanga, utakaopigwa Jumamosi wiki hii au akaja kuwasubiri Dar.

Post a Comment

أحدث أقدم