Kocha Mfaransa amvaa mwamuzi Simba, Yanga


Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Benin, Mfaransa, Didier Nicolle.

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Benin, Mfaransa, Didier Nicolle, amemtupia lawama aliyekuwa mwamuzi wa mezani kwenye mechi kati ya timu yake dhidi ya Taifa Stars, Israel Mujuni Nkongo, kuwa ndiye aliyesababisha wachezaji wake, Baraze Seidou na Adudou Mohamed kupewa kadi za njano zisizokuwa na ulazima.
Benin ilivaana na Taifa Stars kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita na Stars kupata ushindi wa mabao 4-1.Nkongo ndiye mwamuzi atakayesimama kati kuchezesha mechi ya Ligi Kuu Bara, Oktoba 18, mwaka huu kati ya Simba na Yanga, ambaye siku za nyuma aliwahi kuzua kizaazaa wakati akichezesha mechi ya Yanga na Azam.
Mwamuzi huyo aliwahi kufanyiwa fujo na wachezaji wa Yanga mwaka 2012, walipokuwa wakicheza dhidi ya Azam, alisababisha baadhi ya wachezaji wa Yanga kufungiwa na kutozwa faini kutokana na vurugu hizo.
Katika mchezo huo, kikosi cha Benin kilifanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili pasipo Nkongo kujua chochote kwa kuwatoa, Mama Seibou na Dosson Jodel, ambao nafasi zao zilichukuliwa na Baraze Seidou na Adudou Mohamed, jambo lililomfanya mwamuzi huyo kumwita mwamuzi wa kati, Mrwanda,  Hakizimana Louis, ili awape adhabu kwa kuwa walikuwa wamevunja sheria.
Championi lilimshuhudia kocha huyo akimlalamikia Nkongo, mara baada ya mchezo huo kumalizika walipokutana kwenye mlango wa kutokea nje akiwa pamoja na waamuzi waliochezesha mchezo huo.
“Wewe ulikuwa sababu ya wachezaji wangu kupewa kadi za njano, kwa kuwa viongozi wangu walishakuambia kuwa tutafanya mabadiliko,” alisikika akisema kocha huyo mwenye mbwembwe.
Lakini kwa upande wa Nkongo, alisikika akisema kuwa hakuna kiongozi yeyote wa timu ya Benin aliyemueleza kuwa watafanya mabadiliko kwa wachezaji ila alishtuka baada ya kuona wachezaji wapya wakicheza pasipo kuwepo taarifa hali iliyomlazimu kusimamisha mechi ile.
“Hakuna aliyeniambia kuwa mnafanya mabadiliko, nilishtuka kuwa wachezaji wapo uwanjani, kisheria ni lazima nisimamishe mchezo.”

Post a Comment

أحدث أقدم