Ndanda FC yarudi kwao

Dar es Salaam. Ndanda iliyopanda daraja msimu huu inarejea kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kuikabili Ruvu Shooting, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Dennis Kitambi akiwataka mashabiki kuujaza uwanja ili wapate ushindi wa kishindo.
Mechi zote tatu za Ligi Kuu Bara ilizocheza timu hiyo dhidi ya Stand United, Mtibwa Sugar na Coastal Union, imecheza nje ya mkoa wao na sasa itarejea Jumamosi ikipewa nguvu kubwa na mashabiki wao ambao wamepanga kuifunika kabisa Mbeya City kwa ushangiliaji.
Kocha wa timu hiyo, Kitambi aliliambia gazeti hili jana kuwa anaendelea kujifua na kurekebisha baadhi ya makosa yaliyosababisha kufungwa mechi mbili zilizopita.
Kitambi alisema anatambua watakuwa nyumbani hivyo atapata nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki na kuwataka kufika kwa wingi uwanjani kuwapa moyo ili waweze kushinda mchezo huo.
“Tunaendelea na maandalizi yetu vizuri, tumepoteza mechi mbili mfululizo, hilo si jambo zuri lakini hakuna haja ya kukata tamaa kwani ligi bado mbichi tunayo nafasi ya kujipanga ukizingatia sisi ni wageni kwenye ligi.
“Tunachofurahi ni kwamba mechi ijayo tutakuwa nyumbani, tutapata nguvu,” alisema Kitambi.

Post a Comment

أحدث أقدم